Habari Mseto

Mahakama yaamuru mbolea ipimwe katika maabara huru

February 15th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ilikataa kumwagiza Mkurugenzi wa Upelelezi wa Masuala ya Jinai (DCI) George Kinoti kufika mahakamani kueleza sababu ya kukosa kuhudhuria hafla ya kupimwa tena kwa mbolea iliyoingizwa humu nchini Machi 2018 na kampuni ya OCP (K) Limited Ijumaa.

Hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot alisema agizo lililotayarishwa na OCP lilikuwa limeongezewa kwa agizo ambalo mahakama haikuwa imetoa Januari 15, 2019.

Bw Cheruiyot alitupilia mbali ombi hilo la kuitaka mahakama iwaagize DCI na Mkurugenzi wa Shirika la Makadirio ya Ubora wa Bidhaa nchini (Kebs) wafike mahakamani waeleze sababu ya kutoenda bandari ya Mombasa kupata sampuli za mbolea hiyo na kuipeleka katika maabara ya Serikali kupimwa ikiwa iko na madini ya sUmu ya Mercury.

Bw Cheruiyot alisema katika maagizo aliyotoa Januari 15 hakuwa amesema hafla hiyo ya kupimwa tena kwa madini hayo ihudhuriwe na maafisa wa muungano wa mashirika ya uchunguzi.

“Katika uamuzi wangu wa Januari 15 sikuamuru maafisa wa mashirika ya uchunguzi yahudhurie hafla hiyo ya kupimwa tena kwa tani 65,000 za mbolea kutoka Canada kubaini ikiwa iko na madini ya sumu ya Mercury,” alieleza Bw Cheruiyot.

Na wakati huo huo Bw Cheruiyot alimwamuru Meneja Mkurugenzi wa Kebs aandae maabara huru ambapo mbolea hiyo itapipimiwa.

“Maafisa saba wa Kebs wanaoshtakiwa kwa jaribio la kuuawa miongoni mwao meneja mkurugenzi wa zamani Charles Ongwae wanaweza kuhudhuria hafla hiyo ndipo wajifahamishe ikiwa mbolea hiyo ikon a madini ya sumu ya Mercury au la,” aliamuru Bw Cheruiyot.

Bw Cheruiyot pia aliamuru ripoti kuhusu mbolea hiyo iwasilishwe kortini mbali na kupewa washtakiwa.

Ili kuondoa wasiwasi ,hakimu huyo aliamuru OCP itwae agizo lingine ambalo litaidhinishwa na mahakama itakayopelekewa DCI.