Habari

Mahakama yaamuru mbunge Alice Wahome arudishiwe walinzi

July 30th, 2020 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu imemwamuru Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) Hillary Mutyambai amrudishie walinzi Mbunge wa Kandara Alice Wahome.

Jaji James Makau amesema ni kinyume cha sheria kwa IG kuwaondoa walinzi wa mbunge huyo bila kumweleza.

Jaji Makau alisema hakuna ushahidi wowote uliowasilishwa kortini kuthibitisha Bi Wahome alihusika na vitendo vya uhalifu ama kukaidi sheria ndipo walinzi hao watwaliwe.

“Katika kesi hii hakuna ushahidi wowote unaomhusisha mbunge huyu na visa vya uhalifu ama uvunjaji sheria wowote. Pia hajaarifiwa ikiwa anachunguzwa kwa makosa yoyote yanayowezesha kuondolewa kwa walinzi wake,” amesema Jaji Makau.

Jaji huyo amesema madai kwamba Bi Wahome alimsumbua afisa aliyesimamia uchaguzi mkuu eneo la Kandara sio sababu tosha kuwezesha kuondolewa kwa walinzi aliopewa tangu achaguliwe kuwa Mbunge mwaka wa 2013.

Akitoa ushahidi mahakamani, Bi Wahome alisema hawezi kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa wakazi wa Kandara na Kenya kwa ujumla kufuatia kuondolewa kwa walinzi wake.

Alisema anabaguliwa kwa vile wabunge wengine wote wako na walinzi, ni yeye tu hana.

Mwanasiasa huyo mbishi alieleza korti kuondolewa kwa walinzi wake ni njia ya kumtisha asiendelee kuikosoa serikali kutokana na usimamizi mbaya wa masuala ya umma.

Pia alidai msimamo wake wa kumuunga mkono Naibu wa Rais William Ruto mkono umechangia pakubwa katika kutwaliwa kwa walinzi wake.

Walinzi hao waliondolewa Januari 20, 2020, baada ya Idara ya Polisi kusema haitawapa ulinzi maafisa wakuu serikalini wanaojiuhusisha na visa vya uhalifu ama walioshtakiwa hadi kesi dhidi yao zitakapokamilishwa.

Kupitia kwa wakili Stephen Gitonga, Mbunge huyo alisema hatua hiyo ya kumpokonya walinzi ilikuwa ya kumbagua ikitiliwa maanani wabunge wengine wote wako na walinzi kutoka kwa Idara ya Kitaifa ya Polisi (NPS).

Alisema hatua hiyo imehatarisha maisha yake ikitiliwa maanani tangu alipochaguliwa Mbunge 2013 amekuwa na mlinzi.

Bw Gitonga alieleza mahakama kwamba mbunge huyo hajawahi shtakiwa ama kufahamishwa anachunguzwa kwa kushiriki katika uhalifu.

Lakini IG kupitia kwa Mkurugenzi wa Masuala ya Usimamizi NPS Bw Henry K. Borma, mahakama ilijulishwa kufuatia ripoti kwamba Bi Wahome alivuruga amani alipomkejeli afisa wa uchaguzi.

Bw Borma alisema polisi ilifikia uamuzi kuwa maafisa wakuu serikalini wanaohusika na uhalifu wa aina yoyote hawatapewa walinzi kwa vile “huko ni kuwatumia vibaya maafisa wa usalama.”

Mahakama ilifahamishwa kuwa wabunge kujitosa katika utovu wa nidhamu ni ukiukaji wa sheria na kutumia vibaya mamlaka ya walinzi hao.

Bw Borma alisema baada ya tabia ya Wahome kutathminiwa uamuzi ulifikiwa apokonywe ulinzi mnamo Januari 20, 2020.

Katika uamuzi wake Jaji Makau alisema hakuna ushahidi uliowasilishwa kuthibitisha Wahome anastahili kukaa bila mlinzi.

Jaji huyo alisema kuondolewa kwa mlinzi huyo ni kinyume cha sheria kisha akaamuru mwanasiasa huyo arudishiwe walinzi.