Kimataifa

Mahakama yadinda kumruhusu mwanahabari Kabendera kuhudhuria mazishi ya mama yake

January 3rd, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

DAR ES SALAAM, TANZANIA

MAHAKAMA moja nchini Tanzania mnamo Alhamisi ilikataa kutoa ruhusa kwa mwandishi wa habari aliye kizuizini, Erick Kabendera kuhudhuria mazishi ya mama yake, ikisema kwamba waendeshaji mashtaka hawana mamlaka kumwachilia kwa muda mfupi.

Mamake Kabendera, Verdiana Mujwahuzi, alifariki mnamo Desemba 31, 2019, na mpango wa kuutizama mwili wake ulipangwa kufanyika leo Ijumaa katika kanisa moja jijini Dar es Salaam kisha mazishi yafanyike baadaye.

“Erick alikuwa akimtunza mama yake kipindi chote kabla ya kukamatwa kwake. Kwa hivyo, ni muhimu kwake kuhudhuria mazishi, kwa kuzingatia kwamba mama ni mmoja na ni lazima apewe heshima ya mwisho,” wakili wake, Jebra Kambole alisema.

Hata hivyo hatua hiyo ilipingwa vikali na mwendeshaji mashtaka, hata baada ya wakili kuelezea kuwa angesindikizwa na polisi.

Mwandishi huyo alishtakiwa mnamo Agosti 2019 kwa makosa ya ukwepaji wa kodi na utakatishaji wa pesa pamoja na kosa la kupanga uhalifu katika eneo hilo.

Tangu kukamatwa kwake, amekuwa kizuizini akisubiri kesi yake isikizwe na kuamuliwa. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 13.

Kulingana na wadokezi wanaofanya kazi katika vyombo vya habari nchini Tanzania, Kabendera alijikuta pabaya ikiwa ni baada ya kuandika habari ‘hasi’ kuhusu serikali hiyo licha ya madai yaliyosababisha kukamatwa kwake.

Amekuwa kizuizini kwa muda wa miezi mitano sasa na kesi yake imekuwa ikichelewa kortini ama kwa sababu hii au ile.

Serikali ya Rais John Pombe Magufuli imekuwa ikikosolewa na kudaiwa kuwahujumu waandishi wa habari tangu aingie madarakani mwaka wa 2015.

Ni madai ambayo serikali inasema hayana mashiko kwani inajuzu kila mwanahabari kuzingatia taaluma yake.