Habari za Kitaifa

Mahakama yakataa kurefusha agizo la kuruhusu serikali kukata ushuru wa nyumba

January 26th, 2024 2 min read

NA SAM KIPLAGAT

RAIS William Ruto amepata pigo baada ya Mahakama ya Rufaa kukataa kurefusha agizo la kuruhusu serikali kuendelea kukata ushuru wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu.

Majaji watatu wa mahakama hiyo mnamo Ijumaa wametoa hukumu kwamba uamuzi wa kuzingatia matakwa ya umma ni kwamba unaegemea kwa upande wa kutoruhusu ombi la serikali.

“Kwa kuzingatia matakwa ya umma, tunaona haifai kukubali ombi la kurefusha au ombi la kufuta ushuru huo. Uamuzi bora zaidi ni kusubiri hadi kusikilizwa na kuamuliwa kwa maswala yote yaliyoibuliwa katika rufaa,” ikasema sehemu ya uamuzi wa majaji Lydia Achode, John Mativo, na Mwaniki Gachoka.

Soma Pia: Kuna mengi hamjatueleza, wahubiri waambia Ruto na Koome

Mnamo Novemba 2023, serikali ilipata pigo kubwa baada ya Mahakama Kuu kuharamisha sheria ya kuwatoza wafanyakazi na waajiri ushuru wa nyumba.

Agizo hilo la kuzima ushuru huu wa asilimia 1.5 ambao unatozwa kwa kila mfanyakazi na kiwango sawa na hicho kulipwa na mwajiri ilikuwa ni afueni kubwa kwa mahasla.

Kwenye uamuzi wa Mahakama Kuu, Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru nchini (KRA) ilitakiwa kuwarudishia wafanyakazi na waajiri mabilioni ya pesa iliyokuwa imepokea kupitia utekelezaji wa sheria hiyo..

Majaji David Majanja, Christine Meoli, na Lawrence Mugambi walisema bunge lilikosea kuidhinisha ushuru wa nyumba bila kutunga sheria za kuudhibiti.

“Inakinzana na katiba kuidhinisha ushuru wa nyumba ilhali hakuna hazina maalum ya kuweka fedha hizo. Hii mahakama imefikia uamuzi sheria nambari 84 ya sheria za Fedha 2023 inakinzana na Katiba na imeharamiashwa,” hukumu ya majani Majanja, Meoli, na Mugambi ilisema.

Majaji hao walisema wabunge waliidhinisha kinyume cha sheria.

Mahakama ilimkosoa Waziri wa Nyumba kwa kuamuru KRA kupokea pesa kutoka kwa wafanyakazi na waajiri kinyume cha sheria.

“Mamlaka ya KRA imeruhusiwa kupokea ushuru unaokubalika kisheria na wala sio ada ya nyumba kutoka kwa wananchi,” mahakama ikasema wakati huo.

Majaji Majanja, Meoli, na Mugambi waliharamisha kodi hiyo ya nyumba walipotoa uamuzi katika kesi ambapo Seneta wa Busia Okoiti Okiya Omutatah alipinga Sheria ya Fedha 2023 akisema Bunge la Kitaifa lilikosea kuidhinisha kwamba wananchi watozwe ushuru wa nyumba.

Punde tu majaji hao walipotoa uamuzi wao, Mwanasheria Mkuu aliomba agizo hilo lisitishwe kwa muda wa siku 45 kabla ya kukata rufaa.

Bw Omtatah, Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo na Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) kupitia wakili Eric Theuri, walipinga wakisema “mahakama haiwezi kuidhinisha makosa kuendelea kufanyika.”