Habari Mseto

Mahakama yakataa kusikiza mashtaka dhidi ya ndugu wawili

May 26th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

HAKIMU mkuu  katika mahakama ya Milimani Nairobi Francis Andayi  aliamuru kesi ya ndugu wawili wanaokabaliwa na mashtaka ya kujaribu kumlaghai ndugu yao marehemu mali yake yenye thamani ya Sh700 milioni isikizwe na mahakama kuu.

Bw Andayi alitamatisha kesi hiyo ya uhalifu dhidi ya Kulldip Sapra na Ashman Sapra (pichani) a kuamuru kesi hiyo isikizwe na jaji Aggrey Muchelule.

Hakimu alisema kesi hiyo iliwasilishwa kwa ajili ya fitina tu wa mkewe ndugu yao Dkt Nisha Sapra anayekabiliwa na shtaka la kumuua mumewe Yogesh Sapra.

Wawili hao walipinga kesi hiyo wakisema Dkt Sapra alishindwa kuwasilisha ushahidi katika kesi hiyo iliyoko mahakama kuu na akaamua kuivuruga kwa kudai wameghushi stakabadhi za urithi.

Hakimu alisema watoto wa Dkt Sapra walimwandikia barua na pia waliandikia mahakama kuu barua wakisema hawapingi Kuldip na Ashman wakisimamia mali ya baba yao marehemu.

Watoto hao wanasoma nchini Canada na Uingereza.

Bw Andayi alifutilia mbali kesi hiyo akisema “Mahakama kuu ikon a uwezo wa kufutilia mbali cheti cha kuwatambua wawili hao kama wasimamizi wa mali ya Yogesh ikiguduliwa walitumia ukora kuvipata.”

Korti ilisema kifungu cha sheria nambari 68 kinamzuia mshukiwa wa mauaji kudai mali ya marehemu.

Korti ilisema afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP na polisi walikosea kuwashtaki ndugu hao.

Dkt Sapra alikashfiwa kwa kutumia mahakama ya hakimu kuhujumu kesi iliyo mbele ya Jaji Muchelule.

Marehemu Yogesh pamoja na Kuldip na Ashman ni wamiliki wa mali jijini Nairobi na Mombasa.