Na RICHARD MUNGUTI
SERIKALI Ijumaa ilipata afueni mahakama ilipokataa kufutilia mbali agizo kila mwananchi awe amepata chanjo ya Covid-19 kufikia Desemba 21, 2021.
Jaji Antony Mrima aliratibisha kuwa ya dharura kesi ya kupinga agizo la Waziri wa Afya Mutahi Kagwe wananchi wapate chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 uliopelekea mamilioni ya watu kufariki humu nchini na kote ulimwenguni.Akitoa uamuzi, Jaji Mrima alisema hawezi kutoa maagizo ya kupinga wananchi wakipata chanjo ya kuimarisha afya zao.
Alisema afya ni haki ya kila mwananchi kwa mujibu wa Katiba. “Ni jukumu la serikali kwa kila mwananchi kupata huduma za matibabu na kuwa na afya njema. Kutoa agizo la kupinga agizo la kila mwananchi apate chanjo ya Covid-19 itakuwa kukaidi Katiba,” alisema Jaji Mrima.
Jaji huyo aliamuru hati za kesi hiyo zikabidhiwe Waziri wa Afya ajibu madai kwamba hapasi kushurutisha wananchi kupata chanjo hata wale walio buheri wa afya.Jaji Mrima aliamuru kesi hiyo isikizwe Desemba 21,2021.
Kesi hiyo iliwasilishwa na wakili Winfred Otieno Ochieng.