Habari Mseto

Mahakama yakataa Obado kuzuiliwa kwa siku 15

November 16th, 2018 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

GAVANA wa Migori Okoth Obado aliyekamatwa siku mbili zilizopita baada ya bunduki kupatikana nyumbani kwake bila leseni aliachiliwa Ijumaa kwa dhamana ya Sh200,000 pesa taslimu na mahakama ya Kibera, Nairobi.

Hakimu mkuu katika mahakama hiyo Bi Joyce Gandani  alitupilia mbali ombi la upande wa mashtaka kwamba Bw Obado azuiliwe kwa muda wa siku 15 kuwezesha polisi kukamilisha uchunguzi kuhusu silaha hizo.

Akimwachilia Bw Obado, hakimu alisema upande wa mashtaka unaoongozwa na naibu wa mkurugenzi wa mashtaka ya umma Bi Catherine Mwaniki ulishindwa kuwasilisha sababu za kumzuilia gavana huyo.

Hakimu alisema kuendelea kumzuilia mshukiwa huyo kwa tuhuma za kupatikana na bunduki nane nyumbani kwake Migori na Nairobi ni kukiuka haki zake.

Alisema mahakama inaweza tu kumzuilia mshukiwa huyo ikiwa imethibitisha anaweza kuvuruga ushahidi na kutatiza haki ikitekelezwa.

Bi Gandani alisema kuwa hakuna ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka kwamba mshtakiwa anaweza kutoroka.

GAVANA Obado akiwa kizimbani katika mahakama ya Kibera Novemba 16, 2018. Picha/ Richard Munguti

“Hakuna ushahidi wowote uliowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kuonyesha kuwa mshukiwa huyu anaweza kutoroka ama yuko na uwezo wa kuvuruga mashahidi na kutweza haki,” alisema Bi Gandani.

Mahakama ilimwagiza Bw Obado ashirikiane na asithubutu kuvuruga ushahidi kwa njia yoyote ile.

Mawakili Cliff Ombeta , Rogers Sagana Collins Ario wanaomwakilisha  Bw Obado Jumatano walipinga vikali ombi la mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) kupitia kwa Bi Mwaniki azuiliwe kwa muda wa siku 15.

Bw Ombeta alimweleza hakimu kuwa DPP na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) wameendelea kukaidi haki za Bw Obado pasi na sababu.

Bw Ombeta alieleza mahakama kuwa Kifungu nambari 49 cha katiba kimeipa mahakama uwezo na nguvu za kumwachilia mshukiwa yeyote kwa dhamana.

“Mashahidi watakaofika kortini kutoa ushahidi ni maafisa wa polisi na hakuna namna yoyote Bw Obado anaweza kuwavuruga,” alisema Bw Ombeta.

Aliongeza kusema kuwa Bw Obado ni Gavana na anajua athari za kuvuruga ushahidi.

Bw Obado aliachiliwa mwezi uliopita na Mahakama kuu katika kesi inayomkabili ya mauaji ya aliyekuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Rongo Bi Sharon Beylne Otieno.