Habari Mseto

Mahakama yakubali kutazama filamu ya ushoga na usagaji

June 6th, 2019 1 min read

Na SAM KIPLAGAT

SINEMA marufuku ya “Rafiki” ambayo ilizua utata kwa madai inaeneza ushoga, sasa itatazamwa kortini kama sehemu ya ushahidi.

Hii ni katika juhudi zau watayarishaji wake kujaribu kushawishi Mahakama Kuu kuondoa marufuku iliyowekwa na Bodi ya Filamu ya Kenya (KFCB).

Jaji James Makau jana alikubali ombi la Bi Wanuri Kahiu na kampuni ya Creative Economy Working Group la kutaka sinema hiyo kuchezwa kortini.

Jaji alisema kwamba filamu hiyo na marufuku iliyotangazwa mwaka jana ni sehemu ya kesi hiyo.

Mnamo Disemba mwaka jana, Mahakama ilikubali filamu hiyo ambayo inahusu uhusiano wa mapenzi kati ya wasichana wawili itazamwe na watu wazima kwa wiki moja. Hii ilikuwa ni kwa nia ya kuwezesha filamu hiyo kushirikishwa katika tuzo za Oscar.

KFCB ilikuwa imepinga ombi la filamu hiyo kutazamwa kortini ikisema ni ndefu mno.

Wanaoitetea wanasema kwamba ni sehemu ya mwisho ya filamu hiyo ambayo imezua mzozo na KFCB na Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi hiyo Dkt Ezekiel Mutua.

KFCB iliambia mahakama kwamba tukio la mwisho la sinema hiyo na wimbo unaoambatana nayo zinafaa kufutwa kabla ya kuondoa marufuku hiyo.

Bodi ililaumu filamu hiyo kwa madai ya kutetea ushoga na Bi Kahiu akashtaki KFCB na Dkt Mutua kufuatia marufuku hiyo.

Kesi itatajwa Julai 24 mwaka huu.