HabariSiasa

Mahakama yamkausha Baba Yao

July 31st, 2019 2 min read

RICHARD MUNGUTI Na BENSON MATHEKA 

GAVANA wa Kiambu, Ferdinard Waititu Baba Yao, Jumanne alipata pigo baada ya mahakama kumzuia kuingia katika ofisi yake hadi kesi ya ufisadi inayomkabili itakapoamuliwa.

Kwa mujibu wa uamuzi huo, sasa naibu wake Dkt James Nyoro ataanza kutekeleza majukumu ya Bw Waititu.

Saa chache baada ya mahakama kumuagiza Bw Waititu kutoingia katika ofisi yake, Dkt Nyoro alichukua usukani na kufanya kikao na mawaziri wa serikali ya Kiambu.

“Ninaomba kila mtu kutuunga mkono ili tupeleke kaunti yetu mbele kama kaunti nyingine. Tumekosa kupiga hatua kwa sababu ya migawanyiko,” alisema.

Uamuzi huo ni ushindi kwa Dkt Nyoro, ambaye umaarufu wake umekuwa ukiongezeka tangu walipotofautiana mara baada ya kushinda uchaguzi mkuu wa 2017.

Lakini baadhi ya wadadisi walisema uamuzi huo hautamzuia Bw Waititu kuendesha shughuli za kaunti wakisema hakufutwa kama gavana.

Kulingana na wakili Ahmednassir Abdullahi, gavana huyo anaweza kufungua ofisi katika mji mwingine katika Kaunti ya Kiambu na kuendelea na kazi yake.

Bw Waititu amekuwa akimlaumu naibu wake kwa madai ya kutumiwa na maadui wake wa kisiasa kumhujumu, naye Dkt Nyoro amekuwa akimlaumu kwa ufisadi na kutumia vibaya mamlaka yake

Ndoa yao ya kisiasa ilianza kuyumba hata kabla ya siku 100 kuisha baada ya kuapishwa, Bw Waititu akimlaumu Dkt Nyoro kwa kukosoa mbinu zake za uongozi.

Kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa 2017, wawili hao waliungana na viongozi wengine wa Jubilee kuunda kundi lililofahamika kama “United for Kiambu” kumng’oa aliyekuwa gavana William Kabogo.

Dkt Nyoro alikuwa ameacha azma yake ya kugombea ugavana ili kumuunga mkono Bw Waititu.

Baada ya kuapishwa, Bw Waititu alianza kumpuuza naibu wake na kusimamia kaunti peke yake, jambo lililomtenga na viongozi wengine wa kaunti hiyo akiwemo mwakilishi wa wanawake Gathoni Wamuchomba, seneta Kimani Watangi na baadhi ya wabunge.

Viongozi hao waliungana na Dkt Nyoro kukosoa mbinu za uongozi za Bw Waititu wakisema baadhi ya miradi aliyoanzisha ilikuwa ya kupora pesa.

Wadadisi wanasema lengo la Bw Waititu kumhujumu Dkt Nyoro lilikuwa kumsukuma ajiuzulu, lakini mtaalamu huyo wa masuala ya kilimo na chakula alikataa kujiuzulu.

Bw Waititu alikuwa akichunguzwa kwa ufisadi hadi wiki jana Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Noordin Haji alipoagiza akamatwe na kushtakiwa kuhusiana na sakata ya Sh588 milioni.

Siku chache kabla ya Bw Haji kuagiza akamatwe na kushtakiwa, madiwani wa Kiambu waliwaondoa wandani wake kwenye vyeo vya bunge la kaunti akiwemo kiongozi wa wengi Anthony Ikonya, naibu wake Alex Kabuu, kiranja James Kimani Mburu na naibu wake Margret Njeri Gatonye.

Wiki jana, madiwani hao pia walitisha kumtimua spika wa bunge la kaunti Stephen Ndichu ambaye pia ni mwaminifu kwa Bw Waititu.

Akimwachilia Bw Waititu kwa dhamana ya Sh15 milioni, Hakimu Lawrence Mugambi alisema maafisa wakuu serikalini wanaoshtakiwa kwa kupora pesa za umma hawafai kuruhusiwa kurudi kazini na kuendelea kusimamia ofisi walizoshtakiwa kuhujumu.

Mkewe Susan Wangari aliachiliwa kwa dhamana ya Sh4 milioni.

Bw Mugambi alisema ni kinyume cha maslahi ya umma mtu anaposhtakiwa kurudi kazini kabla ya kesi yake kusikizwa na kuamuliwa.

Hakimu huyo alisema sio tu Bw Waititu peke yake ambaye amezuiliwa kurudi kazini katika Kaunti ya Kiambu mbali pia waziri wa ujenzi wa barabara Luka Mwangi Wahinya na wanachama wa kamati wa utoaji tenda Zacharia Njenga Mbugua, Joyce Ngina Musyoka, Simon Kabocho Kang’ethe, Anslem Gachukia Wanjiku na Samuel Muigai Mugo.

Hakimu alisema wiki iliyopita kuwa Jaji Mumbi Ngugi aliamuru Gavana wa Samburu, Moses Lenolkulal asitekeleza majukumu yake hadi kesi inayomkabili ya ufisadi isikizwe na kuamuliwa.

Hakimu Mugambi alisema sheria imewatambua washtakiwa wote kuwa sawa na kuamuru Bw Waititu asirudi kazini hadi kesi inayomkabili isikizwe na kuamuliwa.