Habari Mseto

Mahakama yamkubalia Anne Ngirita kwenda kutibiwa

November 13th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MSHUKIWA mkuu katika kashfa ya NYS Bi Anne Wambere Wanjiku Ngirita Jumanne aliruhusiwa kwenda hospitali na mahakama inayosikiza kesi za ufisadi wa Sh8bn.

Hakimu mkuu Bw Douglas Ogoti alimkubalia Bi Ngirita kwenda hospitali ya Mater kupokea matibabu baada ya kuugua.

Mshukiwa huyo pamoja na mama yake  na dada zake wawili wameshtakiwa kupokea zaidi ya Sh900 milioni kutoka kwa NYS.

Yadaiwa hawakutoa huduma zozote ndipo wapokee pesa hizo.

Bw Ogoti alimkubalia Bi Ngirita kwenda hospitali huku akisubiri ripoti ya Mkurugenzi wa uchunguzi wa Jinai (DCI)  kuhusu ripoti za hospitali alizowasilisha Bi Ngirita.

Bw Ogoti Jumatatu alimwamuru DCI Geoffrey Kinoti achunguze ripoti hizo kubaini ikiwa ni za kweli. Bw Ogoti alimtaka DCI awasilishe ripoti ya rekodi hizo katika muda wa siku tatu.

Atawasilisha ripoti hiyo Jumatano kubaini ikiwa Bi Ngirita ni mgonjwa. Bi Ngirita aliwasilisha rekodi tata za hospitali

Hakimu alitoa agizo hilo alipokataa kuahirisha kesi dhidi ya washukiwa 37 wanaoshtakiwa pamoja na Bi Ngirita kumwezesha kwenda hospitali.

Bi Ngirita aliomba kesi hiyo iahirishwe kumwezesha kwenda hospitali Mater kwa alikuwa mgonjwa na hangeweza kuketi mwa muda mrefu.