Habari MsetoMichezo

Mahakama yamwepushia Kipchoge Keino aibu ya ufisadi

October 19th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANARIADHA mkongwe na bingwa wa zamani wa michezo ya Olimpik Bw Kipchoge Keino aliondolewa aibu Ijumaa kuhusu kashfa ya Sh55 milioni ya michezo 2016 ya Rio baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kuamuru uchunguzi zaidi ufanywe.

Na huenda Kipchoge akateuliwa kuwa mmoja wa mashahidi katika kesi dhidi ya aliyekuwa waziri wa michezo ambaye sasa ni balozi wa Kenya nchini Austria Hassan Wario, aliyekuwa katibu mkuu na sasa balozi wa kenya nchini Urusi Richard Ekai , aliyekuwa kinara wa timu iliyowakilisha Kenya Stephen Spi na washukiwa wengine Mabw Harun Komen, Patrick Kimathi Nzabu na Francis Kinyili Paul almaarufu F K Paul.

Hakimu mkuu mahakama ya Milimani anayemua kesi za ufisadi Bw Douglas Ogoti alifahamishwa DPP amemwagiza Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) achunguze zaidi ushahidi aliokabidhiwa na Bw Keino kupitia wakili wake Bw Cecil Miller.

Bw Ogoti aliamuru kesi dhidi ya Kipchoge itajwe Novemba 16 ndipo DPP aamue ikiwa mwanariadha huyo atajibu mashtaka ya  ufujaji wa Sh18 milioni zilizokuwa zimetengewa wanamichezo waliopeperusha bendera ya Kenya katika michezo ya Olimpiki iliyofanyika mjini Rio De Janeiro nchini Brazil.

Kipchoge anadaiwa akishirikiana na Bw F K Paul waliidhinisha kinyume cha sheria malipo ya ziada Sh15,906,500 kwa wanamichezo kama marupurupu.

Wakili Cecil Miller (kushoto) akiwa na mwenzake Allan Kosgey walipomwakilisha bingwa wa zamani katia riadha Kipchoge Keino mahakamani Oktoba 19, 2018. Picha/ Richard Munguti

Pia ameshtakiwa kumpa mwanawe Bw Ian Kipkosgei Keino Dola za Marekani ($) 24,960 (Sh2,496,000) kusafiri hadi Rio kushabikia michezo hiyo ya kimataifa.

Akieleza sababu ya Kipchoge kutofika kortini, wakili Cecil Miller anayemwakilisha mshtakiwa alisema mnamo Oktoba 17 alimwandikia DPP na kuhoji masuala kadhaa kuhusu malipo ya marupurupu kwa wanariadha.

“Mshtakiwa hakuwa mmoja wa maafisa waliokuwa wanahusika na utoaji wa malipo kwa wanariadha licha ya kuwa mwenyekiti wa kamati ya michezo ya olimpik (NOCK),” Bw Miller alimweleza DPP katika waraka aliomwandikia Oktoba 17.

Bw Miller alidokeza Kipchoge hakuhusika na uendelezaji wa masuala ya usimamizi ya kila siku ya NOCK.

Pia alisema kuwa hakuhusika kamwe na ujumulishaji watu walioandamana na wanariadha hadi Rio nchini Brazil.

Bw Miller aliomba DPP aamuru uchunguzi zaidi ufanywe kuhusu kushirikishwa kwa kikongwe huyu wa michezo nchini.

Mwanawe Kipchoge, Ian Kipkosgei Keino, anayedaiwa alipewa kitita cha Sh2.4 milioni kuenda Rio alikuwa kortini kufuata kesi hiyo dhidi ya baba yake.

Mwanawe Kipchoge Keino, Ian Kipkosgey Keino (kulia) mahakamani. Picha/ Richard Munguti

Kiongozi wa mashtaka Bi Emily Kamau aliambia mahakama DPP ameamuru uchunguzi zaidi kumhusu Kipchoge ufanywe.

Bi Kamau aliomba mahakama impe DPP muda wa siku saba ndipo DCI akamilishe uchunguzi mpya.

“Nimetilia maanani masuala aliyozua Bw Miller katika barua aliyohoji kushtakiwa kwa Kipchoge ilhali hakuhusika kwa njia yoyote na utoaji malipo na kuidhinisha watakaosafiri,” alisema Bi Kamau.

Bw Haji alisema aliisoma kwa makini faili aliyoletewa kuhusu uchunguzi uliofanywa Desemba 2016 na akagundua kuwa  masuala aliyozua wakili Miller hayakuchunguzwa.

“Naamuru DCI achunguze upya kesi ya Kipchoge kisha anirudishie ripoti nitoe mwelekeo,” alisema DPP katika majibu aliyompelekea Bw Miller na ambayo yalikabidhiwa hakimu.

Bw Ogoti aliamuru kesi ya Kipchoge itajwe Novemba 16 ndipo DPP aeleze ikiwa mkufunzi huyo wa riadha atajibu mashtaka au la.