HabariSiasa

Mahakama yaondoa uhuru wa wabunge kufanya watakavyo

May 22nd, 2018 1 min read

Na MAUREEN KAKAH

WABUNGE Jumatatu walipoteza ulinzi ambao umekuwa ukiwaepusha kukabidhiwa stakabadhi za mahakama wakiwa katika majengo ya bunge.

Wabunge pia walipoteza ulinzi wa kutoshtakiwa kuhusiana na matukio katika vikao vya bungeni au kamati za bunge.

Hii ni baada ya Mahakama Kuu kuamua kuwa sehemu za saba na 11 za Sheria ya Mamlaka na Haki za Bunge zinakiuka sehemu za katiba. Jaji John Mativo (pichani) aliamua kuwa sehemu hizo zinakiuka katiba na hazistahili kuwepo.

“Ulinzi wa bungeni si haki ya kibinafsi inayotolewa kwa wabunge ili wajinufaishe kibinafsi bali ni kwa wananchi na mamlaka inayowawakilisha,” akasema Jaji Mativo.

Aliongeza: “Nimepata kuwa sehemu hizi zinaenda kinyume na katiba na sheria kwa kuwa raia mwenye malalamishi hunyimwa uwezo wa kwenda mahakamani kupinga uamuzi unaomwathiri.”

Mahakama ilipata kuwa sheria hiyo haifafanui aina ya maamuzi au ulinzi katika utekelezaji wa majukumu ya wabunge.

Jaji alisema sheria hizo zinazuia utendaji wa haki na kuongeza kuwa katika enzi hizi katiba ni kuu zaidi kuliko bunge, afisi ya rais au mahakama.

Sheria hiyo ilikuwa imeidhinishwa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Julai 21, 2017, ikaanza kutumiwa Agosti 16, 2017 lakini ilikuwa imepitishwa Oktoba 22, 2015.

Machi 2017, rais pia aliidhinisha mswada uliotoa ulinzi kwa madiwani wanapokuwa katika mabunge ya kaunti, sawa na wabunge.