Mahakama yasita kutimua kampuni ya Joho bandarini

Mahakama yasita kutimua kampuni ya Joho bandarini

NA PHILIP MUYANGA

MAHAKAMA kuu imekataa kuitimua kutoka Bandari ya Mombasa kampuni inayohusishwa na aliyekuwa Gavana wa Mombasa Hassan Joho.

Katika uamuzi aliotoa Ijumaa Jaji John Mativo alitupilia mbali kesi ya Chama cha Wafanyakazi wa Bandarini (DWU) iliyoomba korti itimue kampuni ya Portside Freight Terminals (PFT) kutoka Bandari ya Mombasa ikidai kuwa inatekeleza majukumu ya Mamlaka ya Bandari (KPA).

Jaji Mativo alisema kampuni ya PFT inatoa huduma muhimu bandarini na haiwezi kuachishwa kazi jinsi hiyo.

Jaji huyo alisema KPA na PFT zilitia saini mkataba wa kutoa huduma Mei 2020 na imekuwa ikitekeleza kazi zake kulingana na maelewano.

Kulingana na mkataba huo PFT imepewa mamlaka ya kusimamia maeneo mawili katika bandari hiyo.Jaji Mativo alikataa kutamatisha mkataba kati ya KPA na PFT kama alivyoombwa na DWU.

Alitupilia mbali kesi hiyo ya DWU akisema ilishindwa kuwasilisha ushahidi thabiti na wa kuaminika.

Jaji huyo alisema DWU ilikawia muda mrefu kuwasilisha ushahidi kortini kueleza sababu za kutaka PFT itumuliwe bandarini.

DWU haikueleza sababu za kutowasilisha ushahidi katika kesi hiyo na kueleza sababu za kutaka PFT itimuliwe bandarini.

“Hakuna ushahidi wa kuridhisha uliowasilishwa na DWU kuelezea hii korti sababu kilishindwa kuendeleza kesi hii,” alisema Jaji Mativo akitoa uamuzi.

Jaji huyo alisema DWU ilishindwa kabisa kuwasilisha ushahidi katika kesi hiyo na kwamba “mahakama haina budi ila kuitamatisha.”

Jaji huyo alisema mamlaka ya korti hayapasi kutumika kwa njia ya ubatili na akaitupilia mbali kesi hiyo ya DWU.

Mamlaka ya KPA na DWU zilikuwa zimewasilisha kesi zikiomba PTF itimuliwe bandarini zikidai kazi za mamlaka hiyo zitatwaliwa na kampuni hiyo ya Joho.

Mahakama ilitupilia mbali kesi ya KPA iliyoishtaki DWU mnamo Feburuari 2021 kwa kukosekana ushahidi.

Ilipoulizwa na mahakama sababu za kushindwa kuwasilisha ushahidi dhidi ya PTF kwa miezi 13, DWU ilishindwa kutoa maelezo.Wakili wa DWU alieleza mahakama alikuwa na mgonjwa aliyekuwa akimshughulikia ambaye aliaga na kumsababisha msongo wa mawazo.

Mahakama ilielezwa kutowasilisha ushahidi katika kesi hiyo sio kutojali na uzembe mbali ulisababishwa na kugonjeka kwa mtu wa familia ya wakili wa DWU.

Lakini Jaji Mativo alisema wakili wa KPA alieleza korti yeye pamoja na wakili wa DWU wamekuwa wakihusika na kesi nyingine.

“Ufichuzi huu wa wakili wa KPA kwamba walikuwa wakifanya kesi nyinine pamoja yule ya DWU ulibaini hakukuwa na makini ya kukamilisha kesi hii iliyoshtakiwa PTF,” alisema Jaji Mativo.

Aliongeza kusema: “Hakuna sababu ya kuridhisha iliyotolewa kueleza sababu DWU haikuwasilisha ushahidi kwa miezi 13. Hivyo basi kesi ya kupinga PTF kuendelea kutoa huduma bandarini halia mashiko kisheria. Naitupilia mbali.”

  • Tags

You can share this post!

Nassir afunga majaa matatu ya taka

Wazazi kubeba mzigo shule zikifunguliwa kuanzia kesho...

T L