Habari

Mahakama yasitisha hoja ya kumtimua Sonko

March 2nd, 2020 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

HATUA ya bunge la kaunti ya Nairobi ya kumtimua mamlakani Gavana Mike Sonko imepigwa breki Jumatatu na mahakama kuu.

Jaji Byram Ongayo amesitisha majadiliano ya bunge la kaunti ya Nairobi kujadili kumtimua Bw Sonko hadi utaratibu wa kumng’oa mamlakani ufuatwe.

Mahakama ilisema Sonko hakukabidhiwa ushahidi wa makosa anayodaiwa alifanya, pia sahini za madiwani thuluthi moja wanaounga mkono kutimuliwa kwa Sonko hazikuwasilishwa ili zithibitishwe.

Akisitisha mjadala wa kumtimua Sonko, Jaji Byram Ongaya wa Mahakama ya kuamua mizozo ya wafanyakazi na waajiri (ELRC) alisema hoja ya kumjadili Sonko iliwasilishwa kinyume cha mashiko ya kisheria na “haupaswi kuruhusiwa kuendelea.”

Kupitia kwa wakili Harrison Kinyanjui, Sonko, aliwasilisha ombi la kupinga hatua ya kuwasilishwa kwa hoja ya kumjadili kwa lengo ya kumtimua kabisa mamlakani.

Bw Kinyanjui aliomba mahakama isiruhusu mjadala wa kumng’oa mamlakani Bw Sonko kwa vile thuluthi mbili za madiwani waliochaguliwa hawakuwa wameidhinisha hoja ya kumng’oa mamlakaniu uliowasilishwa na Bw Peter Imwatoni

Jaji Ongaya alimruhusu Bw Sonko kuwasilisha ushahidi wa kupinga kujadiliwa kwa hoja iliyowasilishwa katika bunge la kaunti ya Nairobi na mwakilishi wa wadi ya Makongeni Bw Peter Imwatok.

Mjadala katika bunge la kaunti ya Nairobi kuhusu kung’atuliwa mamlakani kwa Sonko ulikuwa umeorodheshwa kujadiliwa leo (Jumanne Machi 3).

Jaji Ongaya alikubaliana na wakili wa Sonko, Harrison Kinyanjui kwamba Bw Imwatok alikaidi sheria za kuthibiti mabunge ya kaunti nambari 67 na 72.

“Hoja ya kujadili kung’atuliwa kwa Sonko itajadiliwa wakati ule itakapowasilishwa kwa mujibu wa Kifungu nambari 67 cha sheria za kudhibiti mabunge ya kaunti,” akasema Jaji Ongaya.

Akiwasilisha ombi la kusitishwa kwa mjadala huo wa kumtoa afisini Sonko, Bw Kinyanjui aliambia mahakama Katibu wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Bw Jackson Ngwele hakukabidhiwa nakala ya kumtimua kazini gavana.

Sheria inasema hoja ya kumtimua Gavana afisini, ombi hilo likipokewa, huwasilishwa kwa Karani mkuu wa serikali ya kaunti ndipo aipeleke kwa Spika kuidhinishwa na Spika wa Bunge hilo.

“Mlalamishi hakupewa nakala ya hoja ya kumtimua kazini kwa mujibu wa sheria,” alisema Kinyanjui.

Bw Sonko alipinga vikali kujadiliwa kwa hoja hiyo akisema haujawasilishwa mahakamani kwa njia ifaayo kisheria.

Lakini Bw Imwatok kupitia kwa wakili wake alisema sheria iwazi kwamba mahakama kuu haipasi kuingilia utenda kazi wa asasi nyingine kuu za serikali.

Jaji Ongayo alifahamishwa mahakama kuu hauna mamlaka kisheria kuingia utenda kazi wa mabunge ya kaunti, bunge la Seneti na Bunge la kitaifa.

“Iwapo hii mahakama itaamua haina mamlaka ya kuamua kesi hii basi itabidi bunge la kaunti ya Nairobi ijadili kung’atuliwa mamlakani kwa Sonko,” mahakama ilielezwa.

Mahakama iliamuru kesi hiyo isikizwe Machi 9, 2020, na kuagiza wahusika wote waandae ushahidi wao na kuuawasilisha kortini.

Hii ni baada ya Sonko kuwasilisha mahakamani ombi akiitaka isitishe mchakato huo wa madiwani wa Bunge la Kaunti ya Nairobi wanaotaka kumwondoa mamlakani.

Sonko amedai hawana nia njema na kwamba mchakato wao haukufuata utaratibu unaofaa.