Habari

Mahakama yasitisha kwa muda ada mpya iliyopandishwa ya uegeshaji magari Nairobi

December 4th, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI na SAMMY WAWERU

MAHAKAMA Kuu imesitisha utekelezwaji wa ada iliyopandishwa ya kuegesha magari jijini Nairobi hadi kesi iliyowasilishwa na Shirikisho la Watumiaji Bidhaa na Huduma Nchini (Cofek) isikilizwe na kuamuliwa.

Cofek iliishtaki serikali ya Kaunti ya Nairobi kwa kupandisha ada ya uegeshaji magari kutoka Sh200 hadi Sh400 kuanzia leo Jumatano, Desemba 4, 2019.

Katika shtaka dhidi ya serikali ya kaunti inayoongozwa na Gavana Mike Sonko, Cofek inasema notisi kwa umma haikuandaa watumiaji magari mapema; haina mashiko, inaadhibu, na ni ya ubaguzi kwa sababu hata umma haukuhusishwa kabla hatua ya kupandishwa ada kufikiwa.

Hii ina maana wenye magari kuanzia leo Jumatano wataendelea kulipa ada ya awali hadi wakati kesi itaamuliwa.

Kesi itasikilizwa Januari 21, 2020.

Baada ya agizo la mahakama wahudumu wa matatu jijini Nairobi wamefurahia uamuzi huo.

Mapema wiki hii, Gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko alikuwa ameongeza ada hiyo maradufu.

Fauka ya ada hiyo kuongezwa kutoka Sh3,650 kwa kila mwezi mmoja hadi Sh5,000 kila mwezi kwa kila matatu ya kubeba abiria 14, wahudumu hawakuongeza nauli kwa wateja.

Bw John Mugo Mwaura, dereva wa KMO Sacco amesema ada hiyo ingewaumiza zaidi Wakenya ikikumbukwa kwamba nayo ada ya bima kwa magari hayo hulipiwa Sh8,200 kwa kila mwezi mmoja.

“Tunalipisha Sh30 kutoka Khoja hadi Aga Khan lakini wenzetu wanaohudumu kutoka barabara ya Latema wanalipisha Sh40,” Bw Derrick Katambani aliye meneja wa Lopha Sacco akasema.

Matatu kadhaa. Picha/ Sammy Kimatu

Bw Katambani amelalamikia hatua ya kuongeza ada hiyo akisema Steji ya Khoja ina mashimo tele yaliyojaa maji huku madereva wakikadiria hasara baada ya magari kuharibika.

Katika Sacco ya Kacose kwenye mzunguko wa Khoja, Msimamizi wa wahudumu, Bw Kamau Gathogo alisema hawajaongeza nauli licha ya tangazo la awali.

“Tuna vituo vinne vikuu hapa jijini ambavyo ni Country Bus, Ngara, Bus Station na Khoja na bado magari ni mengi. Angalia nimevalia buti kujikinga na maji hapa ndani ya kituo. Nina tofauti ngani na mtu wa kukamua ng’ombe,” Bw Githogo akasema.

Katika Likana Sacco madereva wamelalama kuwa kuna msongamano wa magari kila siku katika barabara ya Waiyaki kutoka Limuru.

“Imetulazimu kubuni njia badala tukitumia By-Pass kuunganisha Tigoni/Miritini na Limuru huku ada ikiwa ni Kati ya Sh120 ma Sh150,” Bw Joseph Karanja amesema.

Kwingineko, kumekuwa na nafasi kadha za kuegesha magari waliohojiwa wakidai wenye magari ya binafsi wamekwepa kuyaingiza magari katikati ya jiji kwa kuhofia kulipa ada ya juu.

“Watu wanongopa kulipa pesa nyingu na kuamua kusafiri kwa bas na matatu na kuwacha gari nyumbani,” Dereva wa teksi akasema.