Habari

Mahakama yasitisha ushuru wa 16% kwa muda

September 6th, 2018 1 min read

PETER MBURU na JEREMIAH KIPLANG’AT

MAHAKAMA Kuu ya Bungoma Alhamisi imesimamisha kwa muda kutekelezwa kwa ushuru wa asilimia 16 wa VAT kwenye bidhaa za mafuta.

Hii ni baada ya kikundi cha vijana wa eneo hilo kushtaki waziri wa fedha Henry Rotich kwa kutekeleza sheria hiyo.

Vijana hao walifika mbele ya Jaji Stephen Riech Alhamisi ambapo walipokea amri hizo za kutaka kutekelezwa kwa ushuru huo kusitishwe kwanza.

Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea Septemba 12.

Hatua ya mahakama hiyo imekuja huku kukiwa na mivutano baina ya raia ambao wamelalamika kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha na serikali ambayo iliziba sikio na kuendelea kuweka ushuru huo.

Tangu kuwekwa ushuru huo, bei za mafuta zilipanda, huku petrol ikiuzwa bei ghali zaidi ya Sh129, na kufanya Wakenya kuadhirika baada ya bidhaa za matumizi ya kimsingi na nauli kupanda.

Wakenya pamoja na viongozi mbalimbali wamekuwa wakilalamika kuwa kutekelezwa kwa sheria hiyo hakukufaa wakati huu kwani hali ya maisha ni ngumu mno.

“Gharama ya maisha imepanda sana kwani kila bidhaa ya msingi imekuwa ghali, huku nauli zikipanda. Watoto wanataka tuwape chakula na kuwasomesha na pia nyumba tunafaa kulipa, serikali ifikirie raia wa kawaida,” akasema mkazi wa Nairobi.

Wiki iliyopita wabunge walipitisha mswada wa kuchelewesha kutekelezwa kwa sheria hiyo kwa muda, wakisema hali ya maisha ya Wakenya sasa hairuhusu kuongezewa mzigo wa ushuru.

Aidha, siku mbili zilizopita, kumeshuhudiwa upungufu wa mafuta, huku baadhi ya wahudumu wa usafirishaji wa mafuta wakiingia katika mgomo kususia kutekelezwa kwa ushuru huo.

Vilevile, Tume ya kusimamia sekta ya kawi nchini (ERC) Alhamisi ilitangaza kuwa bei mpya ya mafuta itazidi kutumika kama ilvyopandishwa kuanzia Septemba 1, ikisema kuangaliwa kwa bei hiyo tena ni hadi Septemba 14.