Mahakama yatarajiwa kutoa sababu kamili za kutupilia mbali kesi ya kupinga ushindi wa Ruto

Mahakama yatarajiwa kutoa sababu kamili za kutupilia mbali kesi ya kupinga ushindi wa Ruto

NA RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya Upeo itasoma kesho Jumatatu sababu kamili za kutupilia mbali kesi ya kupinga ushindi wa Rais Dkt William Ruto ambayo iliwasilishwa na kinara wa Azimio Raila Odinga.

Katika arifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Msajili wa Mahakama ya Upeo Bi Leticia Wachira, uamuzi huo utasambazwa kwa wahusika wote kwa njia ya mtandao wa baruapepe Jumatatu saa nane na nusu.

“Nawaarifu kwamba sababu kamili za uamuzi wa kutupiliwa mbali kwa kesi iliyowasilishwa na Bw Odinda na walalamishi wengine saba dhidi ya Dkt Ruto uliosomwa mnamo Septemba 5, 2022 utasambazwa saa nane na nusu kwa njia ya baruapepe kwa wahusika wote na pia kutumwa katika mtandao wa idara ya mahakama wananchi waweze kuusoma,” alisema Bi Wachira.

Jaji Mkuu Martha Koome na majaji wengine sita walitupilia mbali kesi ya Bw Odinga aliyeomba korti iharamishe ushindi wa Dkt Ruto wa uchaguzi mkuu wa Agosti 9,2022 ambapo mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na mipaka (IEBC) Wafula Chebukati alimtangaza mshindi.

Bw Chebukati alimtangaza Dkt Ruto mshindi baada ya kuzoa kura 7.1 milioni dhidi ya kura 6.9 miliioni alizopata Bw Odinga.

Bw Odinga, Seneta wa Busina Okiya Omutata na walalamishi wengine watano walipinga matokeo hayo na kuomba mahakama ya upeo iharamishe ushindi wa Dkt Ruto na kufutilia mbali Gazeti rasmi ya Serikali iliyomtangaza mshindi na kuamuru uchaguzi  wa urais urudiwe katika muda wa siku 60.

Majaji hao saba walifutilia kesi hizo saba wakisema “hakuna ushahidi wowote uliowasilisha kuthibitisha makosa yalifanyika na ukiukaji wa sheria ulikithiri wakati wa zoezi la uchaguzi mkuu Agosti 9, 2022.”

Katika uamuzi uliosomwa na Jaji Koome Septemba 5, 2022 majaji wote saba walikubaliana Dkt Ruto alishinda kwa njia halali na kumwidhinisha kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Kenya.

Baada ya kutupilia mbali kesi hiyo, Jaji Mkuu na Msajili wa Idara ya Mahakama Anne Amadi walimwapisha Dkt Ruto kutwaa hatamu za uongozi wa nchi hii kutoka kwa Uhuru Kenyatta.

  • Tags

You can share this post!

Sitakuwa dikteta, Ruto aondoa hofu

Uhispania watandikwa nyumbani kwa mara ya kwanza baada ya...

T L