Habari Mseto

Mahakama yatoa agizo nyama iharibiwe

July 16th, 2019 1 min read

NA JOSEPH WANGUI

MAHAKAMA imeagiza nyama ya kilo 165 iliyopatikana katika makazi ya mtu binafsi kwenye mtaa wa Asia viungani mwa mji wa Nyeri iharibiwe.

Hakimu Mkuu Mkaazi wa Nyeri Phillip Mutua alitoa amri kwa kiongozi wa mashtaka kuhakikisha nyama hiyo yenye thamani ya Sh65,000 inaharibiwa kutokana na hofu kwamba haifai kuliwa na binadamu kwa sababu za kiafya.

Hata hivyo, Margaret Wanjiku ambaye alifumaniwa nyumbani kwake akihifadhi nyama hiyo aliachiliwa kwa dhamana ya Sh50,000 baada ya kukanusha mashtaka dhidi yake.

Alishtakiwa kwa kuuza nyama isiyokaguliwa, kuendesha biashara bila leseni na kuhifadhi nyama kwenye mazingira machafu.

Afisa wa uchunguzi Sajini Robert Wairi alieleza korti kwamba nyama hiyo ilikuwa imerundikwa ndani ya majokofu mawili kisha kufichwa kwenye chumba cha kulala. Jokofu jingine lilikuwa na sufuria iliyojaa githeri na mtungi wenye maziwa.

Polisi waliwasilisha bidhaa hizo mahakamani kama ushahidi kabla ya hakimu huyo kutoa idhini ziharibiwe.

Wakili wa mshtakiwa, George Gorri alisema msako wa polisi ulikuwa haramu kwa sababu mteja wake alikuwa na kibali cha kuendesha biashara ya kuuza nyama alichopokea kutoka kwa serikali.

Hata hivyo, kiongozi wa mashtaka Pauline Mwaniki alisema uhalali wa kibali hicho kilichotolewa Juni 20, 2019 ulihitaji kuthibitishwa ili ifahamike iwapo mshtakiwa alikuwa akifanya biashara kulingana na sheria ua la.

Kesi hiyo itatajwa Agosti 5, 2019.