Habari Mseto

Mahakama yawavua sita jukumu la usimamizi wa chuo na msikiti Kilifi

July 24th, 2020 2 min read

BRIAN OCHARO na MISHI GONGO

MMILIKI wa msikiti mmoja na chuo katika eneo la Kilifi amepata sababu ya kutabasamu baada ya mahakama kuwashurutisha watu sita waliokuwa na njama za kunyakua majengo hayo kuwatoa katika shughuli za uendeshaji wake.

Watu hao Bw Juma Ali, Hussein Omar, Ghalib Sharif, Bashir Ahmed na Mohammed Bakari waliagizwa kujitoa katika usimamizi wa majengo hayo na Jaji wa mahakama ya mazingira na ardhi Ann Omollo.

Jaji Omollo alisema watu hao hawana haki ya kuendesha shughuli za msikiti huo haliyakuwa mwanawe marehemu alieachiwa jukumu hilo angali hai.

“Mahakama ikikosa kukataza sita hao shughuli ya uendeshaji wa majengo hayo itakuwa imeonyesha asasi hii inawasaidia kunyakua mali ya mwana wa marehemu; hatua ambayo inaweza kusababisha apoteze mali ya baba yake,” akasema.

Akiwasilisha kesi hiyo Bi Fatuma Yusuf ambaye ni mwanawe marehemu Yusuf Avumai Aroi, alieleza mahakama kuwa sita hao walijaribu kuchukua umiliki na usimamizi wa majengo hayo kimabavu kutoka kwake.

Alisema majengo hayo yalikuwa mali ya marehemu babake.

Bi Yusuf alisema mwaka 2013 yeye na kamati yake waliamua kufunga chuo hicho kufuatia ugomvi uliozuka kutokana na uendeshaji wa majengo hayo.

Hata hivyo alisema sita hao walikataa notisi ya kufungwa kwa chuo hicho na kujiingiza kwa nguvu katika majengo hayo kisha kujipigia kura na kujitawaza kama waendeshaji wa chuo hicho.

“Hawakuniomba ruhusa; walivunja kufuli na kujiingiza kwa nguvu kisha kufungua chuo,” akasema.

Aidha alisema sita hao walitengeza barua ghushi iliyoonyesha kuwa marehemu Aroi alikuwa ametoa chuo hicho kwa Wakfu wa Mtwapa.

“Niliwashtaki kwa mahakama ya Kadhi kwa kosa hilo na wakaomba msamaha,” akasema.

Katika ripoti aliyowasilisha katika mahakama, mlalamishi alikanusha kuwa babake alikuwa amekitoa chuo hicho kwa Wakfu na kusema kuwa washtakiwa walitaka kutumia chuo hicho kwa maslahi yao binafsi.

Wakijitetea, washtakiwa walisema Bi Yusuf hakuwa mmiliki wa majengo hayo.

Aidha walikanusha kuwa walijitawaza kama wamiliki au wasimamizi wa majengo hayo.

Bw Bakari ambaye ni babu yake mlalamishi alisema kuwa marehemu alikitoa chuo hicho kwa Wakfu na kupitia Wakfu ndipo msikiti ulijengwa.

“Ni Bi Yusuf aliyetaka kuchukua majengo haya kwa nguvu akiamini kuwa ilikuwa mali ya babake,” akasema Bw Bakari.