Habari Mseto

Mahakama yazima JSC kuchunguza Jaji Mwilu

November 20th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu, IJumaa imezuia hatua ya Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC) kuanza kusikiza ombi la kutaka Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu atimuliwe kazini kwa kukiuka maadili ya kazi.

Jaji James Makau alitupilia mbali ombi la JSC la kutaka kesi mbili alizoshtakiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) zianze kusikizwa.

Jaji Makau alisema maagizo yaliyotolewa Agosti 14, 2020, kusitisha kusikizwa kwa kesi hizo yatasalia hadi Mahakama Kuu itakaposikiza na kuamua kesi aliyowasilisha Jaji Mwilu.

Katika kesi yake, Jaji Mwilu anapinga kesi za kutaka atimuliwe kazini kwa kupokea mkopo wa Sh315milioni kutoka Benki ya Imperial Limited iliyofungwa.

Mwaka uliopita, majaji watano wa Mahakama Kuu walitupilia mbali kesi ya ufisadi aliyoshtakiwa Jaji Mwilu mbele ya Hakimu Mkuu Lawrence Mugambi wakisema haina mashiko kisheria kwa vile ilitokana na masuala ya kibiashara ya kibinafsi.

Baada ya kutupiliwa mbali kwa kesi hiyo, DPP na DCI waliwasilisha ombi katika JSC wakidai Jaji Mwilu alikiuka maadili ya kazi kwa kutumia stakabadhi zilizo na chapa ya idara ya mahakama kuomba mkopo kutoka kwa benki ya Imperial.

Bw Muite anayewakilisha JSC alikuwa ameomba Jaji Makau aamuru kesi hizo mbili zianze kusikizwa na JSC.