Habari za Kitaifa

Mahakama yazuia LSK kufanya uchaguzi wa mwakilishi katika JSC

February 8th, 2024 1 min read

NA SAM KIPLAGAT

MAHAKAMA Kuu imetoa agizo la kusitishwa kwa uchaguzi wa mwakilishi wa mawakili katika Tume ya Huduma za Idara ya Mahakama (JSC), ambao ulikuwa umeratibiwa kufanyika Februari 29, 2024. 

Mahakama imesitisha uchaguzi baada ya wakili Ishmael Nyaribo kuwasilisha mahakamani malalamiko akilaumu bodi ya uchaguzi ya Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) kwa maonevu, baada ya kufungiwa nje asiwanie nafasi hiyo.

Nafasi ya mwakilishi wa kiume wa LSK katika JSC ilivutia wagombea wanne, akiwemo Bw Nyaribo, mwenyekiti wa sasa wa LSK Eric Theuri, Omwanza Ombati, na Prof Michael Wabwile.

Mshindi atajaza nafasi ya Bw Njeru Macharia atakayestaafu mnamo Mei 2024.

Bw Nyaribo alipinga kufurushwa kwake, akisema anakidhi kila hitaji.

“Ninatoa agizo kusitisha uchaguzi huo,” amesema jaji John Chigiti akiongeza kwamba kesi itatajwa mnamo Februari 16, 2024.

Kwenye nakala zake kortini, Bw Nyaribo anadai kwamba haki zake zitakiukwa endapo uamuzi wa washtakiwa kumkataza kuwania nafasi hiyo utadumishwa.

“Pia hali hiyo itaweka mfano mbaya kwa uchaguzi wa LSK siku za usoni,” akasema Bw Nyaribo.