Habari

Mahakama yazuia Mary Wambui kuongoza mamlaka ya kitaifa kuhusu ajira

October 23rd, 2019 1 min read

Na SAM KIPLAGAT

MAHAKAMA ya Masuala ya Leba imemzuia aliyekuwa mbunge wa Othaya Mary Wambui kuongoza Mamlaka ya Kitaifa kuhusu Ajira hadi kesi iliyowasilishwa na Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja isikizwe na kuamuliwa.

Jaji Hellen Wasilwa ametoa agizo hilo Jumatano katika mahakama hiyo katika kesi iliyowasilishwa na Muungano wa Viongozi Vijana Bungeni maarufu kama ‘Kenya Young Parliamentarians Association’.

Katika kesi hiyo ambayo imepigiwa chapuo na Sakaja, walalamishi wanasema Wambui hana sifa, kwa mujibu wa sheria na sera pamoja na uadilifu kikazi, kuwa mwenyekiti wa mamlaka hiyo.

Wambui, kulingana na walalamishi, haafikii hitaji la Kifungu cha 10 (2)(c) cha Sheria ya Mamlaka ya Kitaifa kuhusu Ajira na kwamba hana tajriba ya angalau uzoefu wa miaka saba kusimamia masuala ya wafanyakazi, yaani nguvukazi.

Sifa hitajika za mwenyekiti wa mamlaka hiyo, wanasema, ni za lazima na sharti zifuatwe kuanzia mwanzo hadi mwisho.