Kimataifa

Mahama atangaza atapinga ushindi wa Akufo-Addo

December 10th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

ACCRA, Ghana

RAIS wa zamani wa Ghana, John Mahama ametangaza kwamba atapinga ushindi wa Rais Nana Akufo-Addo katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo mnamo Jumatatu.

Tume Huru ya Uchaguzi ya Ghana mnamo Jumatano ilimtangaza Rais Akufo-Addo mshindi wa uchaguzi huo na sasa atatawala kwa muhula wa pili baada ya kujizolea asilimia 51.59 dhidi ya Mahama ambaye alipata asilimia 47.36.

Ingawa Ghana ni kati ya mataifa thabiti zaidi yanayozingatia demokrasia Afrika, matokeo hayo yalizua taharuki katika ngome za Mahama ambaye alishikilia kuwa uchaguzi huo haukuwa na uwazi.

Pia, Mahama alidai chama chake cha NDC kilishinda viti vingi vya ubunge japo tume bado haijatangaza idadi ya viti kila chama kilijishindia kwenye uchaguzi huo.

“Ushahidi tulio nao unatushawishi kukataa matokeo haya ambayo yametangazwa kwa haraka ili kumpendelea mpinzani wetu,” akasema mbunge wa NDC, Harun Idrissu kwenye kikao na wanahabari.

“Tunapanga kuelekea mahakamani kupinga matokeo ya ubunge na Urais kwenye uchaguzi huu. Raia walitupigia kura kwa wingi na tunaamini sisi ndio washindi. Hatutakubali matokeo haya kamwe,” akaongeza.

Akihutubia maelfu ya wafuasi wake waliokuwa wakisherehekea ushindi wake mjini Accra, Rais Akufo-Addo wa chama cha NPP aliwashukuru kwa kumpa muhula mwingine, akiwataka wadumishe amani.

“Huu ni wakati wa kuungana na kusahau misimamo yetu ya kisiasa. Kipindi cha kampeni kimekamilika na sasa ni muda wa kujenga upya taifa letu,” akasema kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 76. Waangalizi wa kimataifa waliofuatilia uchaguzi huo nao walishikilia kuwa ulikuwa na uwazi mkubwa. Tayari idara ya polisi imetangaza vifo vya watu watano na majeruhi wengine 19 kutokana na ghasia za baada ya uchaguzi.

Mahama, 62, alizua taharuki zaidi nchini humo Jumanne alipodai Rais Akufo-Addo alikuwa anatumia wanajeshi kuhakikisha matokeo ya uchaguzi huo yanampendelea.

“Huwezi kutumia jeshi kujaribu kubatilisha matokeo katika baadhi ya maeneo bunge ambako chama chetu kilishinda. Tutakataa jaribio lolote la kuvuruga matokeo na haki ya raia ya kuwachagua viongozi wao,” akasema Rais huyo wa zamani.

Marais wa Ghana wa miaka ya nyuma wamekuwa wakipokezana mamlaka kwa njia ya amani tangu taifa hilo likumbatie demokrasia zaidi ya miaka 30 iliyopita.

Migogoro kuhusu matokeo ya kura pia imekuwa ikiamuliwa kortini na kila mrengo huridhika na maamuzi yanayotolewa.

Mwaangalizi Mkuu kwenye uchaguzi huo kutoka Bara Ulaya Javier Nart alisema matokeo hayo yalidhihirisha matakwa ya raia na yanafaa kuheshimiwa.