Mahanga adhihirisha uaminifu wa dhati kwa Obado

Mahanga adhihirisha uaminifu wa dhati kwa Obado

Na IAN BYRON

NAIBU Gavana wa Migori, Nelson Mahanga, amedhihirisha uaminifu wake kwa Gavana Okoth Obado kwa kukataa kutwaa uongozi wa kaunti hiyo mara mbili mizozo ilipotokea.

Bw Mahanga ambaye anahudumu chini ya Obado kwa muhula wa pili alikataa kutwaa uongozi wa kaunti hiyo wakati gavana na watoto wake wanne walipokamatwa na maafisa wa uchunguzi wa jinai kwa madai ya kuhusika na ufisadi.

Ingawa hakuwa akijitokeza hadharani sana, Bw Mahanga alizungumza siku moja baada ya kukamatwa kwa Bw Obado na watoto wake wanne na kusisitiza kuwa hakukuwa na pengo la uongozi licha ya changamoto ambazo mkubwa wake alikuwa akipitia.

Hata hivyo, hakutwaa mamlaka kama kaimu gavana lakini aliongoza mikutano ya kamati muhimu za mawaziri wa kaunti akiwasisitizia haja ya kutekeleza ajenda ya maendeleo ya Bw Obado na kupuuza madai kwamba alikuwa akipanga kumuondoa gavana ofisini.

“Niko tayari kutelekeleza majukumu ya mkubwa wangu. Singetaka afungwe jela, ninamuombea na sina nia ya kumuondoa ofisini,” aliambia wanahabari.

Bw Mahanga pia alielezea yake imani kwamba Obado angeshinda masaibu yake na kurejea afisini.

Haya yalijiri huku kukiwa na madai kwamba alikuwa amekotofautiana na Obado na kuacha majukumu ya umma kwa sababu ya kuhujumiwa na mkubwa wake.

Lakini aliporudi, Bw Mahanga alidumisha uaminifu wake kwa Bw Obado akisisitiza kuwa hakuwa na nia ya kumuondoa ofisini.

“Sina nia ya kutwaa wadhifa wa Gavana kwa kuwa hayuko, sikuwa nikihisi vyema hapo mwanzo lakini sasa niko sawa na tayari kushikilia nafasi hiyo. Hakuna pengo la uongozi katika kaunti,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

SHAIRI: Kaozwa mapema bila ujuzi

Kaunti yachukua hatua kudhibiti homa ya dengue