Makala

Mahangaiko: Wakazi wanavyong’ang’ania maji machafu na fisi kwenye bwawa

April 12th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

WAKAZI wa wadi ya Heilu, Kaunti ndogo ya Moyale wanang’ang’ania maji na fisi kwenye bwawa la maji, wakihofia usalama wao na afya yao.

Bi Fatuma Dallo aliambia Taifa Leo kuwa ahadi ya serikali kuwajengea kisima cha maji imesalia hewa na kulazimika kunywa maji machafu yasiyotibiwa.

Serikali ya Kaunti kupitia Tume ya Mgao wa Mapato, mwaka 2019 ilitangaza kuazisha mradi wa Sh100 milioni, uliolenga kuweka sola za kusambaza maji karibu na wakazi.

Mitungi ya wenyeji ikisubiri kuwekewa maji |PICHA |FRIDAH OKACHI

“Mwaka 2018 serikali ilisema itaweka sola na mashine za kusambaza maji nyumbani kwetu ili kuepuka kushambuliwa na fisi,” alisema Bi Dallo.

Mama huyo wa watoto watano alisema maji hayo huwa wanatumia kupikia, kunywa na kufanyia shughuli zingine za nyumbani ilhali si salama kwao.

Pia, alisema wao kutumia maji hayo ni kwa sababu ya kukosa sehemu nyingine ya kuchota maji.

“Ukija mchana hapa, utapata fisi wakinywa maji haya. Wamejificha kwenye huu msitu na hauwezi kuja pekee yako hapa,” alisisitiza Bi Dallo.

“Haya maji ni hatari kwa wageni. Sisi tumezoea kunywa hayo mate ya fisi, wewe ukija hapa unywe utakimbizwa hospitali,” alilalamika mama huyo.

Hata hivyo, jamii hiyo imeweka kamati inayoongozwa na wazee ambao wana orodha ya vijana ambao huongeza urefu wa bwawa hilo na kuweka ua.

Waona hawawezi kusubiri serikali

Vijana kutoka Ethiopia wakipiga gumzo wakati wakuchota maji |PICHA |FRIDAH OKACHI

Mzee wa kijiji Bw Ibrahim Roba Duale alisema bwawa hilo huvuna maji mengi wakati wa mvua kutokana na bidii yao. Kama jamii waliona hawawezi kusubiri serikali.

“Ili kuzuia fisi hao kuja hapa, kamati imepanga vijana wanne au watatu wanaotoa ulinzi hapa. Kisha wanahusika kujenga ua kwa kutumia miti ya kienyeji,” alisema Bw Roba.

Miaka inavyosonga, wanahusisha vijana kutoka taifa la Ethiopia kuteka maji ya familia zao na kufanyia biashara wakati wanatafuta kazi kutoka kwa jamii hiyo.

Mtindo wa awali wa wanawake kufika mtoni pekee yao umebadilika.

“Vijana wetu sio rahisi kuja hapa. Unaona wale vijana wanatoka Ethiopia kuja kutafuta riziki. Na hivyo imepunguza tishio la fisi kula wake zetu na wasichana,” aliashiria Bw Roba.

Waziri wa Maji, Mazingira na maliasili Bw Malicha Boru, aliambia Taifa Leo Dijitali, maafisa wa afya wamekuwa wakizuru katika eneo hilo kuhakikisha usalama wa maji kwa wakazi.

“Maafisa wangu huzuru eneo hilo mara kwa mara kufanya uchuguzi zaidi. Baada ya wiki tatu au tano wana jukumu la kutembelea eneo hilo. Hatuwezi kutaka wenyeji kuathirirwa,” alisema Bw Boru.

Kuhusu usambazaji wa maji nyumbani mwa wakazi hao, utatekelezwa baada ya serikali kutenga pesa.

“Kuna zile sola zilikuwa zimewekwa bado zitafanyiwa marekebisho ili kuwezesha kusambaza maji kwa wakati unaofaa,” alisema Bw Boru.