Akili Mali

Mahangaiko ya mzee aliye na ugonjwa wa matende

June 4th, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

KWA miaka 19 sasa, Mzee Kamande Kamoni amekuwa akiangalia miguu yake ikifura.

Ugonjwa ulimlemea kiasi kwamba miguu ilianza kuwa na uvimbe kama malengelenge na ngozi ikaanza kutoboka huku nyama ya miguu ikioza.

Ilifikia mahali ambapo miguu yake ilianza kutoa harufu mbaya humfanya mzee huyo mwenye umri wa miaka 79 sasa, kutengwa na kunyanyapaliwa.

Bw Kamoni anasema kwamba madaktari wamemuonya kwamba kwa sasa anahitaji kukatwa miguu yote miwili kuanzia sehemu ya magoti kwa gharama ya Sh1.2 milioni.

“Huo ni uamuzi mgumu sana kwangu kwa kuwa sina pesa kiasi hico na pia hata nikizipata, sijui kama nitakubaliana na uamuzi wa kunikata miguu katika uzee huu wangu,” asema Bw Kamoni.

Kile anasema anatafuta, ni kusaidiwa kupata dawa ya kumwezesha kupambana na uvundo wa kuoza kwa miguu yake hiyo na pia dawa ya kuwafukuza nzi na wadudu ambao huzoea vidonda na mizoga.

“Kutembea imekuwa ni vigumu na kila jua linapochomoka, mbali na kuMshukuru Mungu kwa kunipa siku nyingine ya kuishi, huwa ninamuomba aniondolee uchungu, aibu na mahangaiko yanayoletwa na ugonjwa huu wangu,” asema.

Huku akiishi katika kijiji cha Kagongo kilichoko wadi ya Kahumbu iliyoko eneobunge la Kigumo, Kaunti ya Murang’a, Bw Kamoni anasema kwamba umaskini alio nao kwa sasa unamshinikiza kuwa mtu wa kutegemea tu ukarimu wa majirani.

Kwa mujibu wa daktari mkuu katika hospitali ya Murang’a Bw Leonald Gikera, Mzee Kamoni anaugua ugonjwa wa matende ambao kwa lugha ya kimombo ni elephantiasis na ambao kwa sasa katika hali yake hauwezi ukatibiwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa huo husababishwa na viini aina ya minyoo ya familia ya Filariodidea na huenezwa kufuatia mtu kuumwa na mbu walioambukizwa.

“Kile kinachoweza kufanywa ni kudhibiti hali ya kuoza na kunuka. Hali aliyo nayo kwa sasa haiwezi ikabatilishwa na kwa sasa kile tunachoweza kumsaidia nacho ni kumpa afueni ya uhakika ambayo ni kukata miguu hiyo na hatimaye tumwekee mingine spesheli na tumfunze kutembea nayo,” asema Dkt Gikera.

Bw Kamoni anasema umri wake kwa sasa umesonga sana na haoni vile ataweza kujifunza kutembea na miguu ya plastiki ambayo anaambiwa ndio atapewa.

Mzee Kamande Kamoni wakati wa mahojiano. PICHA | MWANGI MUIRURI

Huenda akahitaji ushauri wa mwanasaikolojia, maana anashikilia “chako cha kuzaliwa nacho ni vigumu kukiachilia tu hivi hivi”.

“Hata kikiwa kibaya na ni chako, kipende tu,” asisitiza.

Anasema kwa sasa anashughulika sana na kujipa amani ya roho na kwamba ikifika siku ya kuutoka ulimwengu huu awe amejijengea imani ya kumwezesha kuingia katika ufalme wa milele.

“Miaka niliyo nayo ni ile ya mkondo wa lala salama… hata nipewe hiyo miguu mipya ya mwigo kwani nitatembea nayo kwa miaka mingapi? Kwa sasa juu niko na uwezo wa kujitembeza japo kwa shida, iwapo tu nitapewa dawa za kukausha vidonda nilivyo navyo na hatimaye uvundo huu ulio katika hii miguu ukomeshwe, mimi nitang’ang’ana kuishi na hali yangu hadi pale Mungu ataona kwa neema yake aniite tu,” asema.

Bw Kamoni anasema mikosi imekuwa ikiandama boma lake ambapo pia ana mtoto wake wa kiume ambaye amekuwa kitandani kwa miaka 10 sasa akiwa hajijui na hajielewi.

“Sitaki kusema ni laana au ni urogi. Mimi kama Mkristo nimekubali hali hii jinsi ilivyo na amani ya moyo na mwili huu wangu ndio ambayo ninatafuta. Ule usaidizi ambao ninaweza nikapata nitashukuru sana na katika maombi yangu ya kila siku, nitakuwa nawakumbuka ili msiwahi kujipata katika mahangaiko sawa na haya yangu,” asema.

Mzee Kamoni anasema kwamba “kwa sasa siwezi nikaenda kijitafutia riziki na kazi ni kukaa hapa kwa boma langu nikingojea wasamaria wema waingie waipe roho yangu utulivu”.

Anasema hata kujipeleka hospitalini huwa ni shida “kwa kuwa watu wa pikipiki huogopa kunibeba huku nao wenye magari yao wakinihepa kwa changamoto ya uvundo na wale wadudu ambao hutua kwa vidonda vyangu”.

“Ni shida kubwa lakini kuna daktari ambaye huwa anajitolea kufika hapa kunitibu,” asema.

Anasema daktari huyo amepambana sana hadi kufanya baadhi ya sehemu kadha za miguu yake kukauka na kukoma kuoza huku maumivu yakipungua.

“Lakini hata yeye huniambia suluhu ya kudumu ni kukatwa hii miguu yangu miwili kisha itupwe na badala yake, nipewe mingine ya plastiki,” aungama.

Hata hivyo, Mzee Kamoni anasema kwamba “kuna vile najihisi kuwa ninaweza nikaishi na kutinga umri wa miaka 100.”

“Miaka mingine 21 nikiwa katika hali hii ni utumwa mtupu. Kuna vile ninaweza nikakubali kukatwa… ni ngumu lakini kuna vile ninaweza nikabadili mawazo,” asema.