Habari Mseto

Maharamia wakata mkazi kichwa

September 10th, 2019 1 min read

Na BONIFACE MWANIKI

TAHARUKI imetanda katika Wadi ya Mutha, Kitui Kusini, baada ya maharamia waliojihami kumkata kichwa mwanamume mwenye umri wa makamo na kuwaacha wengine wakiuguza majeraha mabaya huku familia kadha zikitoroka makwao kwa kuhofia usalama wao.

Wavamiajii hao, wanaosemekana kujifanya wafugaji wa Somali, waliripotiwa kuwaua na kuwajeruhi wahasiriwa kufuatia visa vya mara kwa mara vya migogoro kuhusu ardhi ya malisho ambayo imeenea katika eneo hilo kame la Kaunti ya Kitui.

Joram King’ondu, mkazi wa kijiji cha Musenge, alisema maharamia hao, bila kuchokozwa, walimshambulia jirani yake nyumbani kwake na kumkata kichwa Jumapili jioni.

“Tatizo la maharamia eneo hili lilianza miongo kadha iliyopita. Maharamia hao wa jamii ya Somali walimuua babangu na wajomba wangu wawili,” alieleza.

“Watu wametoroka makwa na wanaishi vichakani kama wanyama. Watoto hawawezi kwenda shule kutokana na kuongezeka kwa ukosefu wa usalama. Tunateseka,” alisema King’ondu.

Jonathan Ngau, anayepata nafuu katika Hospitali ya Misheni ya Mutomo, alishambuliwa alipokuwa akiendesha baiskeli na rafikiye na kujeruhiwa vibaya baada ya mmoja wa washambulizi kumdunga kwenye mbavu kwa mkuki.

Katuku Kieti kutoka kijiji cha Ndulani amelazwa katika hospitali hiyo vilevile baada ya maharamia kumvizia alipokuwa akielekea nyumbani kwake jioni.