Dondoo

Mahari ya binti yazulia wazazi zogo

August 24th, 2019 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

BUMULA, BUNGOMA

KIZAAZAA kilizuka katika boma moja eneo hili baada ya polo na mkewe kugombana kuhusu mahari ya binti yao.

Inadaiwa polo alishuku kuwa mkewe alikuwa na njama fiche kuhusu mahari hiyo.

Duru zinasema baada ya binti yao kuwaletea mahari ya ng’ombe 10 na Sh100,000 pesa taslimu, polo alipendekeza waelewane jinsi ya kugawana hela hizo ili kuepuka malalamishi baadaye.

Hata hivyo, inasemekana mkewe alianza kufoka, “Unataka tugawe nini? Huyu msichana nilipambana naye hadi akaolewa. Wewe ulikuwa wapi?”

Hapo polo alishindwa kuzuia hasira zake na akamkaribia mkewe akitaka kumzaba kofi.

“Wewe ni mwanamke sampuli gani. Huyu binti ni wangu na lazima nipate mahari yake,” jamaa alimkaripia mkewe.

Kilichomkasirisha polo zaidi ni safari alizokuwa akifunga mkewe kwenda kwao.

“Tangu mahari iletwe hapa, wewe na watu wa kwenu mmeshikana sana. Kila siku ndugu zako wako hapa na wewe uko kwao. Una nia gani?” jamaa alimfokea mkewe.

Mwanamke naye hakushtuliwa na maneno ya mzee.

“Kama unataka mgao wa mahari tulia. Kiherehere hakitakusaidia,” kipusa alimjibu polo.

Duru zinasema polo alitishia kuwaita wazee wa ukoo.

“Usifikirie utanitawala hapa. Weka pesa zote mezani tujue vile tutagawana. Hawa ng’ombe pia tujue vile tutawalinda la sivyo nitakupeleka kwa ukoo,” polo alidai.

Kipusa alipuuzilia mbali madai ya polo.

“Kwenda huko. Ukoo gani? Nilipomsomesha msichana huyu kazi yako ilikuwa ni ulevi. Acha kujificha kwa ukoo,” akasema.

Polo alilazimika kunyamaza.

“Wewe ukitaka kitu kidogo nitakupa lakini si eti tugawe hii mahari nusu bin nusu,” kipusa alimueleza polo.