Habari MsetoSiasa

Mahindi: Peter Kenneth arai wakulima wakatae bei duni

November 13th, 2018 2 min read


GERALD BWISA na WYCLIFF KIPSANG

ALIYEKUWA Mbunge wa Gatanga, Bw Peter Kenneth, amejitosa kwenye siasa za mahindi na kutaka wakulima wasikubali malipo duni kutoka kwa serikali.

Huku akishauri wabunge kuwasilisha mswada utakaozuia uagizaji wa bidhaa kutoka nchi za kigeni kama bidhaa hizo zinapatikana humu nchini, alisema serikali haifai kujiamulia kuhusu bei itakayonunua bidhaa za wakulima.

Akizungumza Jumamosi alipokuwa Kitale, alitoa mfano wa jinsi uagizaji mahindi kutoka Mexico na mataifa mengine ya nje ulivyosababisha changamoto kwa wakulima wa mahindi ambao sasa wamekosa soko la mazao yao.

“Serikali inafaa ilazimishwe iwe tu ikiagiza bidhaa aina hiyo baada ya kununua mazao yote ya wakulima nchini,” akasema.

Alisema hatua hiyo ya mwaka uliopita ilifanya soko la mahindi nchini lijae kupita kiasi ndipo serikali ikaamua kununua gunia la kilo 90 kwa Sh2,300 kutoka kwa wakulima, ilhali bei ilikuwa Sh3,200 awali.

Kulingana naye, hali hii itaondolea wakulima ari ya kuendeleza kilimo cha mahindi na hata inaweza kuangamiza sekta hiyo.

“Ni makosa kwa mkulima kuagizwa kuhusu bei anayofaa kuuza bidhaa zake. Wabunge wanafaa waungane na waambie serikali kwamba kama haiwezi kununua kwa Sh4,000 basi wakulima hawatauza bidhaa zao,” akasema.

Serikali imekashifiwa vikali kwa kutoa malipo zaidikwa mahindi yaliyoingizwa nchini kutoka mataifa ya kigeni ilhali wakulima wa humu nchini hawapewi bei bora.

“Hata katika sekta ya sukari, hakuna haja kuagiza sukari kutoka nje ilhali wakulima wana miwa mashambani mwao na wameshindwa kuuza,” akasema Bw Kenneth.

Uchunguzi uliofanywa na Wizara ya Kilimo ilionyesha kuwa wauzaji 13 ambao hawakutimiza mahitaji ya kuuzia serikali mahindi waliruhusiwa kuuza bidhaa hiyo kwa maghala ya Eldoret na Kisumu ya Bodi ya Nafaka na Mazao (NCPB). Ripoti ya uchunguzi huo inasema baadhi ya wauzaji walidanganya kuhusu ukubwa wa mashamba wanayomiliki kwani stakabadhi walizowasilisha hazikuwiana.

Ilibainika pia kwamba baadhi ya wauzaji hawakufahamika na machifu kuwa ni wakulima katika maeneo walikodai wanatoka, na inaaminika waliagiza mahindi kutoka nchi za nje wakauzia NCPB huku wakulima halisi wakikosa soko kwa mazao yao.

Bw Kenneth alisema serikali itafanikiwa tu kutimiza lengo lake la uzalishaji wa chakula cha kutosheleza mahitaji ya wananchi kama wakulima watapewa uwezo wa kutosha katika shughuli zao.