Habari

Mahindi ya Uganda yashusha bei ya unga hadi Sh86

August 16th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

BEI ya unga wa mahindi itasalia kuwa chini hasa kutokana na ongezeko la mahindi kutoka nchini Uganda.

Pia, wakulima eneo la Magharibi mwa Kenya walivuna mahindi kwa wingi, hali iliyosababisha bei ya unga kwenda chini.

Pakiti za kilo mbili za unga wa mahindi kwa sasa ni Sh86 katika baadhi ya maduka, ambapo bei hiyo iliuzwa mara ya mwisho mwaka wa 2012.

Bei hiyo imeshuka zaidi ya bei iliyowekwa na serikali ya Sh90 miezi kadhaa iliyopita na iliyobuniwa kudhibiti gharama ya maisha kutokana na kuwa bei ya unga ilikuwa imepanda sana, kiasi kwamba ni watu wachache waliokuwa na uwezo wa kumudu.

Kwa sasa gunia la kilo 90 la mahindi ni Sh2, 000 kutoka Sh3, 200 Januari. Bei mpya ya unga wa ugali ni manufaa makubwa kwa wananchi ikizingatiwa kuwa wengi hutegemea ugali.