Habari MsetoSiasa

Mahindi yaingia siasa za ubabe wa Ruto na Moi

October 1st, 2018 2 min read

BARNABAS BII na STANLEY KIMUGE

CHANGAMOTO zinazokumba wakulima wa mahindi katika eneo la Rift Valley, sasa zimechukua mkondo wa kisiasa huku Naibu wa Rais William Ruto na Seneta wa Baringo Gideon Moi wakijitafutia ubabe kutokana na matatizo ya kilimo hicho.

Chama cha KANU kimeanza kushauriana moja kwa moja na wapigakura kwa kugusia suala tatanishi la kilimo ambalo limekuwa likijadiliwa mno katika maeneo ya Rift Valley siku za hivi majuzi.

Bw Moi, anayeongoza chama hicho, amekuwa akifanya mikutano na wakulima wa mahindi katika Kaunti ya Uasin Gishu ambayo ni ngome ya Bw Ruto, akijikaza kuwashawishi kuhusu hitaji la kufanya mabadiliko ya usimamizi wa sekta hiyo na kuharakishwa kwa utoaji wa Sh3.5 bilioni ambazo wakulima wanadai serikali.

Seneta huyo alifanya mkutano wa karibu saa tano na viongozi mbalimbali na wakulima katika hoteli moja mjini Eldoret wiki iliyopita, saa chache baada ya kuwasilisha mapendekezo yake kuhusu mabadiliko yanayohitajika katika sekta ya kilimo kwa kamati ya Seneti.

Hii ilikuwa ni mara ya pili kwake kuandaa mkutano wa aina hiyo na kusababisha mchechemko wa kisiasa miongoni mwa wafuasi wa Naibu Rais ambao sasa wamelazimika kutafuta mbinu mpya za kuhakikisha Bw Ruto anasalia kuwa kigogo wa siasa za Rift Valley.

“Ni kweli tulikutana na Seneta Moi na tukamweleza malalamishi yetu, na tunatumaini atatuwakilisha vyema katika Seneti kwa sababu tunataka sera zitakazotusaidia zibuniwe. Alituahidi pia kwamba ataitisha mkutano mwingine hivi karibuni,” akasema Kimutai Kolum, mmoja wa wakulima waliohudhuria mkutano huo.

Hata hivyo, Bw Ruto alipokuwa katika Kaunti ya Nandi wiki iliyopita aliwahakikishia wafuasi wake kwamba atakuwa kwenye debe kuwania urais 2022 na akapuuzilia mbali madai kwamba umaarufu wake unadidimia katika eneo hilo.

“Msiwe na hofu kwani kila kitu kiko sawa na mnafaa kujiepusha na aina yoyote ya siasa za mgawanyiko, na badala yake tuweke macho yetu kwa lengo tunaloazimia,” akasema.

Tofauti na Bw Moi, Naibu wa Rais amekuwa akiwasiliana na wapigakura kupitia kwa viongozi wa kisiasa walio wandani wake ambao humpelekea ripoti nyumbani kwake Sugoi katika Kaunti ya Uasin Gishu au Karen jijini Nairobi.

Katibu Mkuu wa KANU, Bw Nick Salat, alisema chama hicho kimeamua kuwasiliana moja kwa moja na wananchi ili kutatua matatizo yanayowakumba kwani hakuna anayewatetea ipasavyo kwa sasa.

“Kuna pengo la uongozi katika eneo hili na tunahitaji mtu wa kulijaza. Kile ambacho chama chetu kinafanya ni kuhakikisha watu wetu wanaheshimiwa hata tunapoendelea kutetea maslahi yao,” akasema Bw Salat.

Malipo ya wakulima wa mahindi katika eneo la Rift Valley yamecheleweshwa kutokana na sakata ambapo Bodi ya Nafaka (NCPB) inadaiwa kununua mahindi kutoka kwa wafanyabiashara walioyaagiza kutoka Uganda na wakalipwa pesa zilizopasa kutumika kuwalipa wakulima wa humu nchini.

Sakata hiyo ilipelekea baadhi ya wakuu wa NCPB kuondolewa huku pia kukiwa na madai kuwa wanasiasa kadhaa wa eneo hilo wakiwemo wabunge walihusika katika kashfa hiyo.

Hali hiyo imewafanya wakulima kuvunjika moyo na pia kuhisi kuwa serikali inapuuza maslahi yao.