Michezo

Mahrez afunga matatu na kusaidia Man-City kudhalilisha Burnley ligini

November 29th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

RIYAD Mahrez alifunga mabao matatu kwa mara ya kwanza ndani ya jezi za Manchester City mnamo Novemba 28, 2020 na kusaidia waajiri wake kudhalilisha Burnley 5-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (Bundesliga) ugani Etihad.

Mahrez ambaye ni raia wa Uingereza alifungulia Man-City karamu ya mabao katika dakika ya sita kabla ya kuongeza la pili kunako dakika ya 22.

Benjamin Mendy alikamilisha kwa ustadi krosi ya kiungo Kevin de Bruyne na kufungia Man-City goli la tatu katika dakika ya 41. Bao hilo lilikuwa la kwanza kwa Mendy kuwahi kufungia mabingwa hao wa EPL mnamo 2017-18 na 2018-19.

Sajili mpya Ferran Torres alipachika wavuni bao la nne la Man-City katika dakika ya 66, sekunde kadhaa kabla ya Mahrez kuzamisha kabisa chombo cha wageni wao kwa kufunga goli la tano na lake la tatu.

Ushindi huo ulikuwa mnono zaidi kwa Man-City kuwahi kusajili hadi kufikia sasa katika kampeni za EPL msimu huu. Ilikuwa mara ya kwanza kwa Mahrez kufunga mabao matatu katika mechi moja tangu afanye hivyo dhidi ya Swansea City mnamo Disemba 2015 wakati akichezea Leicester City waliotawazwa mabingwa wa EPL mnamo 2015-16.

Burnley walitegemea huduma za kipa Bailey Peacock-Farrell katika mchuano huo kwa kuwa mlinda-lango chaguo la kwanza Nick Pope anauguza jeraha.

Baada ya De Bruyne kushuhudia kombora lake likigonga mwamba wa goli, refa alikataa kuhesabu mabao yalifungwa na Torres na Gabriel Jesus kwa madai kwamba wawili hao wakikuwa wameotea kabla ya kutikisa nyavu za wageni wao.

“Ilikuwa muhimu kusajili ushindi mnono na wa kuridhisha katika mechi hii baada ya kupoteza mechi ya awali kwa mabao 2-0 dhidi ya Tottenham Hotpsur,” akasema kocha Pep Guardiola huku akiwa mwingi wa sifa kwa De Bruyne aliyeridhisha zaidi katika safu ya kati.

Man-City walijibwaga ugani wakilenga kujinyanyua baada ya kufunga mabao 10 pekee kutokana na mechi nane za ufunguzi wa kampeni za EPL msimu huu. Kwa mujibu wa Guardiola, idadi hiyo ndogo ya mabao imechangiwa na majeraha ambayo yamekuwa yakitatiza mafowadi wake tegemeo – Sergio Aguero na Jesus.

Man-City kwa sasa wamefunga jumla ya mabao 27 katika michuano sita iliyopita dhidi ya Burnley uwanjani Etihad. Miamba hao kwa sasa wanajiandaa kupepetana na FC Porto ya Ureno kwenye gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Disemba 1 huku Burnley wakialika Everton kwa mchuano wa EPL mnamo Disemba 5, 2020.

MATOKEO YA EPL (Novemba 28, 2020):

Brighton 1-1 Liverpool

Man-City 5-0 Burnley

Everton 0-1 Leeds United

West Brom 1-0 Sheffield United