Michezo

Mahrez anusia tuzo ya mchezaji bora kikosini Man City

November 1st, 2018 1 min read

NA CECIL ODONGO

MCHEZAJI ghali zaidi kwenye kikosi cha mabingwa watetezi wa ligi kuu nchini Uingereza Manchester City, Riyad Mahrez ameteuliwa miongoni mwa wachezaji watakaowania tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Oktoba, 2018 klabuni humo.

Ingawa alianza mwezi huo kwa kupoteza penalti muhimu dakika za lala salama Manchester City walipokutana na Liverpool ugani Anfield Oktoba 7, Mahrez aliyejunga na City kutoka mabingwa wa zamani Leicester City mwanzoni mwa msimu wa 2018/19 alijizoazoa na kubeba timu yake katika mechi zilizofuatia.

Mwanasoka huyo alikuwa mhimili mkubwa kikosini kwenye ushindi dhidi ya over Hoffenheim ya Ujerumani ugenini katika mechi ya kuwania klabu bingwa barani Uropa.

Mahrez,27 alifuata hayo kwa kufuma wavuni bao safi katika ushindi wa mechi ya EPL Burnley kisha kutoa pasi murwa iliyochangia bao la ushindi dhidi ya Shahtar Donetsk katika ligi ya klabu bingwa Uropa.

Jumatatu Oktoba 29 winga huyo alikuwa moto wa kuotea mbali baada ya kuonyesha kiwango cha juu cha kabumbu na kufunga bao lililowarejesha Mancity kileleni mwa jedwali la EPL.

Ingawa hivyo, Mahrez ambaye amewahi kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka anakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa midfilda David Silva na mlinzi Aymeric Laporte ambao pia walifanya kweli kwa kutambisha timu mwezi Oktoba.