Michezo

Mahrez anyakua king'asti mwingine baada ya talaka

February 6th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

RIYAD Mahrez ametema mke wake Rita Johal na bila kupoteza hata sekunde amejinyakulia mwanafunzi wa fasheni Taylor Ward.

Mwezi Desemba 2019, Mahrez, 28, alisikitishwa na Rita baada ya ripoti kuwa mwanamuziki huyo alidondokwa na mate kuwaona mabondia Anthony Joshua na Deontay Wilder.

Mshambuliaji matata wa Algeria Mahrez na Muingereza Rita,25, walifunga pingu za maisha katika harusi ya kisiri mwezi Agosti 2015. Walibarikiwa na mtoto msichana Inaya Mahrez.

Hata hivyo, mwanamitindo Rita, ambaye ana asili ya Kihindi, alipotea njia alipomtupia jicho Joshua katika kilabu cha usiku cha Tape London.

Rita na Joshua walionekana wakicheka na kutongozana, huku mkono wa Rita ukipapasa goti la bingwa huyo wa uzani wa “heavy” duniani wa mataji ya WBA, IBF, WBO na IBO.

Japo Joshua, ambaye ni kapera baada ya kutengana na mchezaji densi Nicole Osbourne mwaka 2016, anasemekana alikataa Rita baada ya kufahamishwa ni mali ya Mahrez.

Ripoti hizo zilikuwa za kutonesha kidonda cha Mahrez kwani mwezi uliotangulia uvumi ulienea kuwa Rita alionekana na bingwa wa dunia za uzani wa “heavy” wa taji la WBC Muamerika Wilder katika kilabu cha usiku cha Club Liv mjini Manchester.

Habari hizo zilifanya Mahrez kutengana na Rita kabla ya vyombo vya habari nchini Uingereza kuripoti mapema Februari 2020 kuwa Mahrez,28, ametaliki Rita rasmi na kujinyakulia Taylor, 22, lakini baada ya “kubusu vyura” wengi tu.

Mahrez, ambaye mwaka 2019 pia aligonga vichwa vya habari alipoamrishwa na mahakama kulipa yaya wake wa zamani Catalina Miraflores Sh470,814 baada ya kupunguza mshahara kwa njia isiyo ya haki, alipeleka Taylor na marafiki wake 15 katika karamu ya jioni ya kukata na shoka.

Alikomboa chumba binafsi katika hoteli ya Ivy Asia mjini Manchester na kulipa bili ya Sh654, 000 katika karamu hiyo.

Wawili hao waliwahi kuonekana pamoja wakitoka katika eneo la wageni mashuhuri katika kilabu cha usiku cha China White mnamo Desemba 31, 2019. Ripoti zinasema kuwa wameshaambia familia zao pamoja na marafiki kuhusu uhusiano wao. Inasemekana Taylor alimpa Mahrez sharti la kuwa hawatahusiana kimapeni hadi pale atakuwa amewacha rasmi mke wake.

Taylor aliwahi kuhusishwa na mvamizi matata wa Argentina Sergio Aguero, ambaye pia anachezea Manchester City, pamoja na nyota wa Everton, Mason Holgate.

Babake Taylor, Ashley Ward, 49, ni mchezaji wa zamani wa Manchester City na Leicester, ambayo pia Mahrez alichezea kabla ya kutua uwanjani Etihad.