Habari Mseto

MAHUBIRI: Yesu yu pamoja nasi siku zote, usihofu chochote

April 7th, 2024 1 min read

NA PADRI KAMUGISHA

ASIYEKUWEPO na lake halipo. “Tunapokombolewa kutoka katika hofu zetu, uwepo wetu moja kwa moja unawakomboa wengine,” alisema Nelson Madiba Mandela.

Bwana Yesu alipofufuka na kukutana na mitume, Mtume Tomaso hakuwepo. “Walakini mmoja wa wale Thenashara, Tomaso, aitwaye Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu.” (Yohana 20:24).

Yesu, mwenye moyo wa huruma, yupo pamoja nasi hadi ukamilifu wa dahari.

Kuna aina nyingi za kutokuwepo: Kwanza ni kutokuwepo kimwili. Mtu hayupo kabisa haonekani. Tomaso hakuwepo kimwili. Siku hiyo alikosa baraka za Yesu mfufuka.

Pili ni kutokuwepo kihisia. Baada ya siku nane Yesu alipowatokea mitume Tomaso alikuwepo kimwili na kihisia. Kwa hisia alitamka, “Bwana wangu na Mungu wangu.”

Tatu, ni kutokuwepo kisaikolojia, yaani mawazo yako mbali. Bila shaka kisaikolojia kabla ya kutokewa na Bwana Yesu Tomaso hakuwa pamoja na mitume, hata kama alikuwa nao kisaikolojia alikuwa mpweke.

Katika msingi huu yeye alikuwa mbali na mambo yake.

Nne, ni kutokuwepo kiroho, kiimani. Tomaso alipoambiwa kuwa Yesu Kristo amefufuka, hakuamini.

“Uko wapi?” (Mwanzo 3:9). Ni swali la kwanza ambalo Mungu alimuuliza binadamu alipoasi katika shamba la Edeni.

Kutokuwepo katika ibada, mikutano ya kidini kunamfanya mtu kuulizwa: uko wapi?

“Kutokuwepo kwa baba kunaiathiri familia vibaya katika malezi ya watoto,” alisema Papa Fransisko, Furaha ya Upendo, Na. 55.

Kwa upande mwingine, kuna familia ambapo baba yupo lakini muda mwingi haonekani nyumbani.

Athari za kutokuwepo kwake ni watoto kuhisi wapweke kama yatima. Kiasi cha baba kutojua tabia za wanawe na hata kukosea majina yao.

Naye mama husumbuliwa na maswali ya watoto wakitaka kujua baba yuko wapi.

Athari nyingine ni mama kulemewa na majukumu ya malezi kwani watoto wanamdai kila kitu.

Mama pia anaweza kupata kishawishi cha kwenda nje ya ndoa maana mpenzi wake hana muda naye. Nayo maendeleo ya kustawisha familia yanakosa dira, mwelekezi.