Siasa

Maina Njenga: Ilitabiriwa mimi kuwa ‘kingpin’ Mlimani

January 18th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

ALIYEKUWA kiongozi wa kundi haramu la Mungiki, Maina Njenga, sasa amedai kuwa kuna utabiri uliotolewa kwamba “mimi ningekuja kuwa kiongozi na msemaji wa kisiasa wa eneo la Mlima Kenya”.

Bila kutoa ufafanuzi zaidi, Bw Njenga alisema kuwa utabiri huo umeanza kutimia.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio mnamo Jumatano, Bw Njenga alisema kuwa kama njia ya kutimiza ‘utabiri’ huo, amejitolea kuwakomboa kisiasa wakazi wa ukanda huo.

“Mimi ninafuata timio la utabiri uliotolewa kwamba hatimaye mimi ndiye nitachukua uongozi wa kisiasa wa ukanda huu. Ndipo nimeamua kujitosa kwenye juhudi za kuwakomboa vijana wetu,” akasema Bw Njenga.

Kauli hiyo, hata hivyo, inaonekana kutofautiana na semi zake za hapo awali, ambapo amekuwa akidai kuwa kiongozi wa kisiasa wa ukanda huo ni Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Kulingana na wadadisi, huenda Bw Njenga ameanza kujipigia debe, baada ya Bw Kenyatta kujitenga na mkutano aliokuwa ameuandaa katika uwanja wa Kabiru-ini, mjini Nyeri, Desemba 31, 2023.

“Kuna uwezekano kuwa Bw Njenga anataka kuendesha siasa zake kwa njia huru, bila kumhusisha Bw Kenyatta. Pia, huenda huo ukawa mkakati wa wawili hao kutoonekana hadharani, japo kiuhalisia ni kuwa bado wako pamoja,” asema mdadisi wa siasa James Waithaka.

Bw Njenga, hata hivyo, alikanusha madai ya kupata ufadhili wowote wa kisiasa kutoka kwa Bw Kenyatta ili kuendesha harakati zake za kisiasa.