MAINGI: Wanawake wanaowania nyadhifa za uongozi wasidhulumiwe, wasihangaishwe

MAINGI: Wanawake wanaowania nyadhifa za uongozi wasidhulumiwe, wasihangaishwe

Na NDUNGI MAINGI

WANAWAKE ambao wamejitokeza kuwania nafasi tofauti za uongozi wanafaa kuboreshewa mazingira yao wakati wa maandalizi, usajili wa vyama na mchakato mzima wa uchaguzi.

Ni jukumu la serikali na mashirika ya utetezi wa haki na jinsia kuhakikisha kwamba wanawake wako huru kufuata ndoto zao kikamilifu bila kuingiliwa wala kubaguliwa kwa vyovyote vile, hadi mchakato mzima ukamilike.

Wakati huu juhudi za wanawake kukwea kwenye nyadhifa za uongozi zinazidi kuimarika, jambo ambalo litachangia katika kuimarisha usawa wa kijinsia na kupinga udunishwaji wa wanawake kutoka kwa baadhi ya wanajamii wanaishikilia mielekeo ya kijadi.

Kwanza, viongozi wa vyama wanapaswa kuhakikisha kwamba wanawake hawajabaguliwa wakati wa kuchagua wawaniaji wa nafasi tofauti za uongozi kwa tiketi za vyama husika. Wanafaa kupewa nafasi sawa na wanaume na sifa zinazofaa kuzingatiwa.

Wanawake pia wanahitaji kupigwa jeki wakati wa kampeni, kupitia misaada ya kifedha na vile vile kisaikolojia. Baadhi ya wanawake hupitia hali ngumu wakati wa kampeni kwa kukosa hela za kutosha kuendesha shughuli hizi.

Vita dhidi ya wawaniaji wa kike pia vinafaa kukabiliwa, ili kuhakikisha kuwa wako salama kila wakati. Njama za kuwavamia wanawake zinafaa kukabiliwa ili visa hivyo visije vikashuhudiwa kwa vyovyote, kama nyakati za awali.

Kwa mfano, ripoti ya Shirikisho la Mawakili wanawake(FIDA) ya 2014 ilieleza kuwa wawaniaji wa kike walikabili wakati mgumu hadi baadhi wakahiari kujiondoa kwenye kinyang’anyiro, ikiwemo kutokana na kushambuliwa.

Matusi na maneno ya kuwadhalilisha wanawake pia yasiruhusiwe katika vuguvugu la kuwania uongozi. Baadhi ya viongozi wa kiume wanapokumbana na wapinzani wa kike hutumia maneno ya kuwadunisha kama njia ya kujipigia kampeni. Wanaotumia maneno ya kichochezi kwa misingi ya jinsia wachukuliwe hatua za kisheria.

Viongozi pia, hasa wale wa kike wana jukumu kubwa la kukabiliana na kundi linaloendesha mila za unyanyaswaji wa wanawake. Kuna makundi yanayowashauri na hata kuwalazimisha wanawake kupashwa tohara au kuingia kwenye ndoa za mapema.

Isitoshe, jamii zenye mielekeo ya kijadi kuhusiana na nafasi za uongozi kwa wanawake zinfaa kuelimishwa, ili kubadili mitazamo hii hasi. Nyingi za jamii hizi ni zile zinazotoka mkoa wa Kaskazini Mashariki nchini.

Baadhi ya jamii bado zinaamini kuwa nafasi ya mwanamke ni jikoni, na daima anafaa kuwa chini ya mwanamume. Kwa baadhi yao, uongozi na nafasi ya mwanamume na wanawake hushutumiwa kwa kujitosa katika ulingo huo.

Takwimu zinaonyesha wazi kuwa wanawake wako tayari ‘kuondoka jikoni’ kikamilifu kutokana na mabadiliko katika nyadhifa za uongozi tangu uchaguzi wa kwanza chini ya katiba mpya mnamo 2013.

Mwaka huo, wanawake hawakupata nafasi yoyote katika useneta au ugavana. Mnamo 2017, walipata nafasi tatu katika nyadhifa hizo mbili, huku mafasi zaidi zikitarajiwa wakati huu, ambapo wengi wametangaza nia yao ya kuwania nyadhifa hizo.

You can share this post!

Karo: Magoha aonya walimu akiwataka kutofukuza wanafunzi

Arsenal yakubali kutoa Sh7.8 bilioni ili kumng’oa...