Michezo

Mainz wamfuta kazi kocha Achim Beierlorzer

September 30th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

KIKOSI cha Mainz kinachoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kimemfuta kazi kocha Achim Beierlorzer siku 10 tangu msimu mpya wa kivumbi hicho kuanza.

Kutimuliwa kwa Beierlorzer kunafanyika katika wiki ambapo wanasoka wa Mainz walisusia vipindi vya mazoezi baada ya fowadi Adam Szalai kupigwa marufuku na kuambiwa atafute kikosi kipya cha kumpa hifadhi.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Ujerumani, Szalai aliongoza wanasoka wenzake kushiriki maandamano ya kudai malimbikizi ya mishahara ambayo hawakulipwa katika miezi ya kwanza ya mkurupuko wa virusi vya corona.

Hata hivyo, klabu imekana madai hayo na kusisitiza kwamba sababu za Szalai kuambiwa aondoka Mainz ni za kispoti. Mainz walipokezwa kichapo cha 4-1 kutoka kwa Stuttgart katika mchuano wao uliopita ligini mnamo Septemba 26, 2020.

Beierlorzer, 52, alipokezwa mikoba ya Mainz Novemba 2019 na nafasi yake kwa sasa itatwaliwa na aliyekuwa msaidizi wake, Jan-Moritz Lichte kwa muda mfupi kabla ya kocha wa kudumu kupatikana.

“Nimefadhaishwa sana na maamuzi ya Mainz. Hata hivyo, naitakia klabu hiyo kila la heri katika vibarua vilivyopo mbele,” akasema Beierlorzer.

Anakuwa kocha wa pili kufutwa kazi katika Bundesliga kufikia sasa msimu huu baada ya David Wagner kupigwa kalamu na Schalke 04 kwa sababu ya matokeo duni ya kikosi chake.

Wagner, ambaye pia amewahi kuwanoa Huddersfield nchini Uingereza, ametimuliwa na Schalke baada ya kikosi hicho cha Bundesliga kupoteza mechi mbili za kwanza za msimu huu wa 2020-21.

Kupigwa kwa Schalke katika michuano hiyo miwili ligini, kuliendeleza rekodi duni ambayo imewashuhudia wakikosa kusajili ushindi katika jumla ya mechi 18 zilizopita tangu mwisho wa muhula wa 2019-20.

Schalke walipondwa 8-0 na mabingwa watetezi Bayern Munich katika mechi ya ufunguzi wa msimu huu kabla ya kupepetwa 3-1 na Werder Bremen mnamo Septemba 26.

Wagner, 48, alijiunga na Schalke mnamo 2019 baada ya kushawishiwa kuagana na Huddersfield aliowanoa kwa zaidi ya miaka mitatu.

Wasaidizi wake Christoph Buhler na Frank Frohling pia wamefurushwa na Schalke uwanjani Veltins Arena.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO