Makala

Maisha mtihani

March 1st, 2019 2 min read

Na MWANDISHI WETU

VISA hivi tumevichapisha tu kwa ajili ya kutoa hamasisho.

Kwa kawaida mahakama huwa zinawachukulia watoto kwa huruma na hata adhabu dhidi ya wanaokosea kuwa za kiwango cha chini.

Hata hivyo, katika visa kadha vya kipekee, korti zimelazimika kuwaadhibu vikali watoto ambao walikuwa wakora ama majambazi hasa, baada yao kufanya makosa ambayo yalishangaza.

Aaron Campbell, 16

Mvulana huyu wa miaka 16 kutoka Scotland alipatikana na hatia ya kunajisi  kisha kuua mtoto wa miaka sita, Alesha MacPhail katika kisiwa cha Bute, mwaka 2018.

Baada ya kumuua, Aaron aliripotiwa kuutupa mwili wa mtoto huyo msituni, ukiwa na majeraha 117.

Hata hivyo, licha ya kuwa sheria inaelekeza kuwa watoto wa chini ya miaka 18 wasitambulishwe hata wanapokosea kwa kuwa hali hiyo inaweza kuathiri kukua kwao, Jaji Lord Matthews aliamrisha kuwa mvulana huyo anafaa kutajwa na kuaibishwa.

Jaji huyo alisema “Siwezi kufikiria kuhusu kesi katika visa vyote enzi hizi ambayo imechukiza kiasi hiki. Vyombo vya habari vinaweza kuchapisha jina na picha zake.”

Katika visa kadha visivyo vya kawaida, majaji wameonekana kuelekeza watoto waliokosea na kupatikana na hatia za makossa makubwa ya jinai yaliyoshangaza kutambulishwa kwa umma.

Thompson na Venables

Wawili hawa walikuwa na umri wa miaka 10 wakati walimwiba mtoto wa miaka miwili nje ya duka la nyama eneo la Bootle, Merseyside mnamo 1993 mamake mtoto huyo alipoingia dukani kuchukua kitu.

Hata hivyo, maiti ya mtoto huyo ikiwa imejeruhiwa vibaya ilipatikana kwenye reli eneo la Wlaton, Liverpool siku mbili baadaye. Mtoto huyo alikuwa na majeraha 22 kichwani na 20 katika sehemu zingine za mwili yaliyosababishwa na chuma na matofali 27.

Mnamo Novemba 1993, Thompson na Venables walipatikana na hatia ya kumuua mtoto huyo na wakatupwa jela hadi wahitimu miaka 18.

Japo wawili hao walikuwa wakirejelewa kama mtoto A na mtoto B kesi ilipokuwa ikiendelea, walipopatikana na hatia, jaji Morland aliruhusu vyombo vya habari kuwaanika kwa kutaja majina yao.

Jaji huyo alisema, “Nilifanya hivi kwani haki ya umma kujua ilizidi ile ya washukiwa. Kulikuwa na haja ya umma kufahamu na kujadili kuhusu makossa yanayofanywa na watoto wachanga.”

Hata hivyo, wawili hao baadaye waliachiliwa kutoka jela, japo iliwabidi kubadili majina kwa amri ya korti, ili waweze kuishi bila kuathiriwa na matendo yao ya utotoni.

Mary Bell

Msichana huyu kutoka Newcastle alishangaza taifa hilo wakati mnamo 1968 aliwanyonga hadi kufa wavulana wawili katika eneo la Scotswood.

Mary alikuwa na umri wa miaka 10 pekee na aliwaua watoto hao, Martin Brown aliyekuwa na umri wa miaka minne Bell alimnyonga ndani ya nyumba, kisha miezi miwili iliyofuata akamnyonga Brian Howe aliyekuwa na umri wa miaka mitatu.

Baada ya kuua mtoto huyo, alimkata miguu na tumbo kwa kutumia wembe na makasi.

Kortini, Mary alihukumiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia (manslaughter) kwa misingi kuwa alikuwa mtoto na hivyo hangewajibika kikamilifu.

Uchunguzi wa korti ulibaini kuwa mtoto huyo alionyesha dalili za matatizo ya kiakili. Katika kipindi chote cha kesi, alikuwa akitajwa na hata alipohukumiwa akaangaziwa sana na vyombo vya habari.

Mnamo 1980, Mary aliachiliwa kutoka gerezani baada ya kufungwa jela miaka 12, lakini akapewa jina jipya kutokana na hali kuwa la kwanza tayari lilikuwa limeharibika sana. Baadaye aliendelea na maisha yake kama kawaida.

William Cornick

Alipokuwa na umri wa miaka 15, William alimdunga kisu hadi kufa mwalimu wake katika chuo cha mafunzo lugha ya Kihispania.

Alifungwa miaka 20 jela baada ya kesi ya kisa hicho cha 2014 kukamilika.