Habari MsetoSiasa

Maisha ya Gakuru yangeokolewa, asimulia dereva

June 28th, 2019 1 min read

Na JOSEPH WANGUI

DEREVA wa aliyekuwa Gavana wa Nyeri, marehemu Wahome Gakuru (pichani) Alhamisi alieleza jinsi ajali iliyomuua gavana huyo ilifanyika katika barabara kuu ya Nairobi-Kenol.

Bw Samson Kinyanjui ambaye alikuwa akimwendesha Dkt Gakuru katika gari hilo aina ya Mercedes lilipopata ajali eneo la Makenji asubuhi ya Novemba 7, 2017 aidha alilaumu idara za uokoaji kwa utepetevu.

Kulingana naye, wakati gari lilipoteza mwelekeo na kugonga bati zito kando ya barabara, bati hilo lilipenyeza ndani ya gari na kuchomoza hadi nyuma, gari likisonga kwa mita 66.

Alisema wakati huo mguu wake ulikuwa umekwama katika sehemu ya kukanyaga mafuta gari lizidi kusonga.

Bw Gakuru ambaye alikuwa amekaa siku 77 pekee afisini tangu kuchaguliwa alikaa garini akivuja damu na kwa uchungu takriban dakika 45, wakati umma na wasaidizi wake walikuwa wakijaribu kumwokoa.

“Kifo chake kilisababishwa na hali ya timu za uokoaji kukosa kufika kwa muda uliofaa. Maisha yake yangeokolewa. Hakuna juhudi zilizofanywa kumuokoa. Baada ya kupambana, nilienda chini ya gari na nikamuinua kisha akatolewa na umma,” akasema Bw Wanyaga, alipokuwa akitoa ushahidi katika kesi hiyo, mbele ya Hakimu Wendy Kagendo.

Alisema gari hilo halikuwa na matatizo ya kiufundi kwani lilikuwa limekaguliwa, kinyume na madai aliyotoa gavana wa kaunti hiyo wa sasa Mutahi Kahiga, ambaye alikuwa naibu wake.

Siku chache baada ya kifo cha Dkt Gakuru, Bw Kahiga alidai kuwa gari hilo lilikuwa na matatizo na kuwa yeye alikuwa amelazimika kutoa gari lake litumiwe na Dkt Gakuru.

Lakini dereva huyo alisisitiza kuwa gari hilo lilikuwa katika hali nzuri, akiongeza kuwa marehemu gavana huyo alikuwa akibadilisha madereva mara kwa mara.

Kabla ya Bw Wanyaga, Dkt Gakuru alikuwa amehudumu na madereva watatu tofauti, kwa kipindi alichokuwa afisini.

Kabla ajali hiyo kutokea, gari lenyewe GVN 019A halikuwa limetumiwa kwa wiki moja na lilikuwa katika makazi yake katika mtaa wa Ring Road.