Afya na Jamii

Maisha ya wanawake na watoto hatarini kwa uhaba wa chanjo

May 18th, 2024 2 min read

ANGELA OKETCH Na MERCY CHELANGAT

WATOTO 1.6 milioni na idadi sawa na hiyo ya wanawake waja wazito na wasichana 750,000 wa chini ya umri wa miaka 10 wanakabiliwa na hatari ya kukosa chanjo muhimu baada ya serikali kukosa kununua dawa hizo.

Hii ni kutokana na deni la Sh4.6 bilioni inayodaiwa na shirika moja la kimataifa linalouza chanjo dhidi ya maradhi kama kama vile, Kifua Kikuu, Polio, Surua miongoni mwa mengi yanayoathiri watoto na akina mama wajawazito.

Aidha, kulingana na stakabadhi zilizoonekana na Taifa Jumapili, Kenya haijanunua chanjo ya DTP (Diphtheria, Tetanus, Pertussis) kwa muda wa miezi 10 na tayari hospitali nyingi zinakabiliwa na uhaba.

Vile vile, chanjo ya BCG ambayo hupewa watoto wanapozaliwa kuzuia kifua kikuu, haijanunuliwa kwa muda wa miezi minane iliyopita. Tayari chanjo dhidi ya magonjwa kama vile kupooza (Polio), Kifua Kikuu, Surua, Homa ya Manjano, Malaria na ile ijulikanayo kama Human Papillomavirus (HPV) zimeisha.

Nchini Kenya, chanjo ya HPV hupewa wanafunzi wa kike, walio chini ya umri wa miaka 10 na ambao idadi yao ni 750,000, kila mwaka.

Aina hii ya chanjo zilizosalia katika baadhi ya vituo vya afya haiwezi kudumu kwa muda wa mwezi mmoja. Nchi yoyote ile inahitajika kuwa na akiba ya kila moja ya chanjo hizi ambazo zinaweza kudumu kwa angalau miezi minane.

Lakini akiba ya chanjo iliyoko sasa haiwezi kudumu kwa zaidi ya miezi miwili.

Uhaba uliopo sasa unasababishwa na uhaba wa pesa au serikali kuchelewa kutoa fedha za kununua chanjo hizo kwa wakati.

Kulingana na rekodi za Wizara ya Afya, ni watoto 15,000 pekee walipewa chanjo hizo kutokana na uhaba huo.

“Kupungua kwa idadi ya watoto wanaopewa chanjo nchini kutachangia kutoa kwa milipuko ya magonjwa hayo yanayoweza kuzuiwa. Hali hii imewaka maisha ya mamilioni ya watoto hatarini na kuchangia ongezeko la watoto wanaokufa mapema, sawa na watu wazima,” kulingana stakabadhi iliyowasilishwa kwa Wizara ya Afya.

Kupungua kwa idadi ya watoto wanaopewa chanjo na ongezeko la idadi ya watoto na akina mama wanaokabiliwa na hatari ya maradhi hayo, huenda likapandisha gharama ya huduma za afya kupitia matibabu ya magonjwa na matatizo mengine yanayosababishwa nayo.

Hii inaathiri afya ya wahusika kwa surua huweza kusababisha upofu na polio inaweza kusababisha ulemavu na hata kifo.

Kenya imekuwa ikishuhudia milipuko ya surua tangu mwaka jana.

Kufikia sasa zaidi ya visa 1,052 vya ugonjwa huu vimeripotiwa katika kaunti za Turakana, Mombasa, Samburu, Kilifi, Garissa, Meru, Nairobi, Kwale na Wajir.

Mwaka huu, serikali ilipunguza mgao wa bajeti kwa ajili ya ununuzi wa chanjo kutoka Sh2.6 bilioni hadi Sh1.2 bilion.

Hatua hiyo imechangia kushindwa kwa serikali kulipa malimbikizi ya madeni inayodaiwa na shirika la Gavi na uhaba wa chanjo. Shirika hili la kimataifa linaidai serikali ya Kenya kitita cha Sh4.2 bilioni.

Isitoshe, serikali inadaiwa Sh500 milioni na shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto (Unicef) ambalo hununua chanjo na kuzisambaza katika hospitali za umma kwa niaba ya serikali ya Kenya.

Kaimu Mkurugenzi wa Afya Dkt Patrick Amoth amethibitisha kuwa kuna uhaba mkubwa wa chanjo nchini kwa sababu serikali imechelewa kulipa Gavi Sh4.2 bilioni.