Habari MsetoSiasa

Maisha yangu yamo hatarini – Alice Wahome

January 15th, 2020 1 min read

Na NDUNGU GACHANE

MBUNGE wa Kandara, Alice Wahome amedai kuwa maisha yake yamo hatarini kwa kumkosoa Rais Uhuru Kenyatta.

Mbunge huyo alisema alipokea simu wiki iliyopita kutoka kwa mwanamume aliyemtishia maisha yake akisema anapaswa kukimbilia usalama wake.

“Baadhi ya viongozi kutoka mrengo wa Kieleweke wanataka kuniua na endapo wakazi wa eneobunge langu watanikosa, hao ndio wanapaswa kuhojiwa kuhusu nilipo,” aliwaeleza wafuasi wake mjini Kandara alipotoa hundi za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi.

Alidai kumekuwa na mikutano inayopangwa na Mbunge wa Kuteuliwa Maina Kamanda na Mwakilishi wa Wanawake wa Muranga, Sabina Chege kuhusu jinsi ya kuvuruga hafla zake.

“Walikuwa wametuma wahuni kujaribu kuvuruga hafla yangu ya kutoa hundi za ufadhili wa masomo lakini majasusi wetu wakawatambua na tukawaita polisi waliokamata watu 22 miongoni mwao,” akasema Bi Wahome.