Habari Mseto

Maiti ya kitoto malaika yatupwa karibu na ofisi ya umma

February 3rd, 2024 1 min read

NA ALEX KALAMA

HUZUNI imetanda mjini Malindi katika Kaunti ya Kilifi baada ya maiti ya mtoto mchanga kupatikana imetupwa kando ya barabara karibu na ofisi ya naibu kamishna mnamo Ijumaa.

Wakiongozwa na Bi Selina Mwaka, wakazi wamelaani hatua ya aliyetekeleza kitendo hicho huku wakitoa wito kwa wanawake kuchukua majukumu ya ulezi kikamilifu.

“Tumeona kitu kimeefunikwa na hatukujua ni nini hadi tulivyochunguza na kugundua mtoto kimalaika alikuwa ametupwa kando ya barabara hii,” akasema Bi Mwaka.

Alisema ni jambo la kusikitisha mno wa sababu “ukifanya hivyo, jua kuna mwenzako anahitaji mtoto”.

“Tujikazeni wanawake tulee hawa watoto wetu. Anayehisi ugumu aende mbele kwa serikali ili kujieleza kwamba hawezi kumlea mtoto wake, kuliko kumtupa,” akaongeza.

Wakazi hao wameitaka serikali ya kaunti hiyo kuboresha usafi wa mazingira ya barabara aliyotupwa mtoto huyo ili kudhibiti visa kama hivyo siku za usoni.

Kwa upande wake Bw Enock Kalume, ameiomba serikali kumchukulia hatua kali za kisheria mtu aliyetenda kitendo hicho endapo atapatikana.

“Aliyetekeleza unyama huo alimtupa pahala pachafu ajabu kiasi cha kuwa yule mtoto hata kule kuvuta hewa huenda ndiko kulisababisha kifo,” akasema Bw Kalume.

Mkazi mwingine, Bw Thomas Hanga, amesistiza haja ya manispaa ya Malindi kuboresha usafi barabara zote zilizo mjini humo.

“Kama halmashauri ya manispaa ya baraza la mji wa Malindi itachukulia kwa uzito jambo hili na kulifanyia kazi kwa kusafisha barabara zote za ndani ya mji, matukio kama haya yatadhibitiwa,” akasema Bw Hanga.

Alitaka barabara ya kutoka majengo ya bunge la kaunti kuelekea Kanisa la Jesus Celebration Centre (JCC) nayo pia kusafishwa.