Habari Mseto

Maiti ya mwanachuo mjamzito yapatikana msituni

September 5th, 2018 1 min read

JUSTUS OCHIENG’ na PETER MBURU

POLISI Kaunti ya Homa Bay wana kibarua kigumu kuchunguza na kufahamisha Wakenya watu walioteka nyara mwanahabari wa Nation kutoka kaunti hiyo, kisha kumuua mwanafunzi wa chuo kikuu.

Mwanahabari wa kampuni ya Nation Media Group Barack Oduor alitekwa nyara Jumatatu jioni na watu walioshirikiana na msaidizi wa Gavana Okoth Obado, katika mazingira yanayohusishwa na habari aliyokuwa akiandaa kuhusiana na ufisadi kaunti hiyo.

Bw Oduor alisema msaidizi huyo wa Gavana Obado, Michael Oyamo alimhadaa kuwa angempa habari za kusaidia kuandaa taarifa yake, kabla ya kubadilika na kumwacha mikononi mwa wahuni waliotaka kumuua.

Mwanahabari huyo aliokoka kifo baada ya kuruka kutoka gari lililokuwa likiendeshwa kwa kasi la watekaji nyara hao, huku akibaki na majeraha mabaya mwilini.

Kwa bahati mbaya, mwanadada waliyekuwa naye Oduor, Bi Sharon Otieno, mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo kikuu cha Rongo, na ambaye alikuwa mja mzito aliuawa na wanyama hao na mwili wake kupatikana usiku wa Jumanne.

Sharon walitekwa nyara pamoja na Barack, lakini akabaki kwenye gari pale mwanahabari huyo aliporuka.

Babake, Bw Douglas Otieno Jumatano alidhibitisha kuwa aliuona mwili wa bintiye katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya Oyugis Level Four saa saba usiku.

Alieleza Taifa Leo alifika hospitalini baada ya kufahamishwa na polisi kuwa mwili wa mwanamke ulipatikana ukiwa umetupwa msituni.

Bw Oyamo (msaidizi wa Gavana Obado) alitiwa mbaroni Jumanne kuhusiana na kisa hicho.

Lakini wazazi wa Sharon sasa wamebaki na huzuni tele, huku mamake akishindwa kuwasiliana na Taifa Leo kutokana na kilio.

Kampuni ya Nation Media Group pamoja na muungano wa wanahabari (KUJ) umetaka polisi kuharakisha uchunguzi wao na kuwachukulia hatua za kisheria wale waliohusika.

“Vitisho na mavamizi hayatazuia wanahabari kueleza kuhusu ufisadi uliokita na ukosefu wa uaminifu katika kaunti hizo mbili ambazo hazina matunda yoyote ya ugatuzi,” akasema Bw Erick Oduor, katibu mkuu wa KUJ.