Habari

Maiti ya mwanamume yapatikana katika choo cha kanisa Kakamega

August 10th, 2019 1 min read

Na SHABAN MAKOKHA

[email protected]

MAAFISA wa polisi Kakamega wanachunguza kisa ambapo mwili wa mwanamume umepatikana Jumamosi asubuhi katika choo cha kanisa.

Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Kakamega Central, David Kabena amesema mwili huo wa mwanamume ambaye hajatambuliwa umepatikana saa nne asubuhi katika Christian Gospel Church mtaani Otiende.

“Tumefahamishwa na Askofu Patrick Mwayilwa Shivali kwamba ameukuta mwili huo chooni. Maafisa wa polisi wamefika mahala hapo na kupata mwili huo ukining’inia kwa shati katika dari la choo hicho,” amesema Bw Kabena.

Amesema hakuna stakabadhi za utambulisho za mwendazake huyo ambaye washiriki wa kanisa hilo wamekiri kwamba wamekuwa wakimuona kanisani siku mbili zilizopita ijapokuwa hawakumjua ni nani.

“Tumeanzisha mchakato wa kumtambua pamoja ili tufahamishe jamaa zake pamoja na kubaini kiini cha kifo chake. Kwa sababu alikuwa akining’inia, hatuwezi tukaondoa uwezekano wa yeye kujitoa uhai. Hata hivyo, ni upasuaji wa maiti utakaotupa picha halisi ya kifo chake,” amesema Bw Kabena.

Maiti imepelekwa katika Hospitali Kuu katika Kaunti ya Kakamega.