Habari Mseto

Maiti ya Okoth yateketezwa Kariokor

August 3rd, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

MWILI wa Mbunge wa Kibra Ken Okoth umeteketezwa Jumamosi katika makaburi ya kuchomea maiti ya Kariokor huku mamake akikosa kuhudhuria akisema itikadi za kiutamaduni hazimruhusu kufanya hivyo.

Akizungumza na wanahabari, jamaa wa familia hiyo, Bw Evans Oluoch amefichua kwamba mamake Okoth, Bi Angeline Ajwang Okoth, alisisitiza hadi dakika ya mwisho kwamba maiti ya mwanawe Okoth ilipaswa kuzikwa na wala sio kuteketezwa.

“Kwa kweli familia haikukutana kwa sababu ikiwa ingekutana mamake Ken angakuwepo hapo pamoja na baadhi ya watu wa familia. Tulisikia habari hizo tu jana kupitia runinga wakati Sifuna aliposema familia ilikuwa imekubaliana kumteketeza Ken na nimeshtuka kwa sababu hata mamake hakuhusishwa kamwe,” amesema Bw Oluoch.

Aidha, amefichua kwamba kiongozi wa ODM Raila Odinga alikuwa amekubali kutoa ndege ambayo ingeusafirisha mwili wa Okoth.

Ni ahadi ambayo haikutimia.

“Baadhi ya jamaa hawakuja Nairobi kwa kuwa walifahamu fika kwamba mwili ulikuwa ukielekea Kabondo. Mipango ilikuwa tayari imeanza na kila kitu kilikuwa kimeandaliwa. Tulishtuka mambo yalipobadilika ghafla Ijumaa jioni. Tulifahamishwa kwamba mwili utateketezwa jambo ambalo mamake Ken alipinga vikali. Kwa kweli alitaka mwili uzikwe kando na nyumba yake,” amesema akiongeza kwamba uamuzi wa kuuteketeza mwili wa Okoth ulifanywa na jamaa wawili wa familia pamoja na mjane Monica Lavender Okoth.

Kuzika mgomba

Kulingana na Oluoch, ni kutokana na tukio hilo ambapo mamake marehemu, Bi Ajwang, hakuwa na hiari ila kuamua atazika mgomba kuashiria kumzika mwanawe mpendwa.

“Mamake Okoth atasafiri kuelekea Kabondo baadaye leo (Jumamosi) ambapo mnamo Jumapili anatarajiwa kuzika mgomba wa ndizi eneo la Kabondo Kasipul, kitendo kitakachoashiria alimzika mtu aliyempenda mno,” amesema kwa majonzi.

Oluoch alimwelekezea kidole cha lawama mjane wake Okoth kwa kusisitiza uteketezaji wa marehemu licha ya familia yake kupinga hatua hiyo akisema hakuna jamaa wa familia hiyo aliyekuwa ameona wosia wa mbunge wa Kibra uliosema mwili wake uteketezwe baada ya kukata roho.

Aidha, Oluoch alipuuzilia mbali jamaa ya babake Okoth kutoka Rangwe akisema kamwe hawajawahi kujishughulisha na familia ya mwendazake.

Isitoshe, alifichua kwamba familia hiyo ilifahamu vyema kuhusu kuwepo kwa mtoto wa kiume wa marehemu, Jayden Okoth pamoja na mamake anayedaiwa kuwa mpenzi wa siri wa Okoth, Anne Muthoni Thumbi.

Familia ya marehemu imeandamwa na misukosuko punde baada ya kifo chake huku misururu ya visa ikizuka kimoja baada ya kingine hali ambayo imezidishia uchungu na huzuni wa wafiwa.