Habari Mseto

Maiti yarudishwa mochari kwa kukosa kulipiwa mahari

August 30th, 2018 1 min read

NA KALUME KAZUNGU

WAOMBOLEZAJI katika kijiji kimoja eneo la Baharini, tarafa ya Mpeketoni, Kaunti ya Lamu Alhamisi waliachwa vinywa wazi pale maiti iliyokuwa ikitayarishwa kuzikwa ilipoamriwa kurudishwa mochari.

Mwili wa Bi Damaris Kanini, 18 ulilazimika kurudishwa kwenye hifadhi ya maiti ya hospitali ndogo mjini Mpeketoni baada ya wazazi wa marehemu kutofautiana na wakwe zao kuhusu ni wapi alikostahili kuzikwa msichanana wao ambaye alikuwa ameolewa miezi minane pekee kabla ya kufariki.

Duru zinaarifu kuwa hatua ya wazazi wa marehemu kukataa msichana wao kuzikwa kwa wakwe zao inatokana na kwamba alikuwa hajalipiwa mahari yoyote.

Mzee wa mtaa mtaa wa eneo hilo Moses Kinuthia ambaye pia ni bavyaa wa marehemu alisema awali walikuwa wameafikiana na familia ya mwendazake kwamba msichana wao azikwe kwa mumewe.

Waombolezaji wakitazama kaburi likifunikwa baada ya mazishi kutibuka kufuatia mzozo kati ya familia mbili kuhusu ni wapi marehemu angezikwa kijijini Baharini, tarafa ya Mpeketoni, kaunti ya Lamu. Picha/ Kalume Kazungu

“Mimi ni mzee wa mtaa na pia baba wa kijana aliyeoa marehemu. Awali nilikuwa nimeafikiana na wazazi wa mkaza-mwana kwamba maiti izikwe kwetu.

Tunashangaa kwamba kaburi limechimbwa na yalikuwa karibu kufanyika na kisha ghafla tunaambiwa kuna amri ya korti inayokataza mazishi kuendelea. Tumejaribu kusuluhisha kwa ofisi ya naibu kamishna wa hapa lakini imeshindikana. Tayari tumerudisha maiti mochari na tunasubiri tutakachoambiwa na wenzetu,” akasema Bw Kinuthia.

Aidha waombolezaji waliokuwa wamejitokeza kijijini hapo kwa mazishi walikasirishwa na hatua ya kurudishwa kwa maiti mochari, jambo ambalo liliwafanya kuifunika kaburi iliyokuwa imetayarishwa.

“Kamwe hatujaridhishwa na kitendfo cha leo. Huu ni mkosi kwetu na tumeifunika kaburi yote. Hawawezi kutupotezea wakati kuchimba kaburi tukitarajia kufunika mwili na kisha tunaambiwa mazishi hayatafanyika,” akasema Bw Samuel Kimani.

Naye Bw Emmanuel Wanyoike ambaye ni mmoja wa viongozi eneo hilo alisema kuna haja ya familia kusuluhisha mizozo yao kwanza kabla ya kuchukua hatua yoyote ili kuzuia aibu.