Michezo

MAJABALI: Senegal, Super Eagles waanza vyema safari

November 15th, 2019 3 min read

Na MASHIRIKA

SENEGAL na Nigeria zilikuwa kati ya timu zilizoanza kampeni ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (Afcon) mwaka 2021 kwa kishindo.

Licha ya nyota wa klabu ya Liverpool, Sadio Mane kubanwa vilivyo dhidi ya Congo Brazzaville, Teranga Lions ilitumia uwanja wake wa nyumbani wa Lat Dior mjini Thies kuponyoka na ushindi wa mabao 2-0 katika mechi ya Kundi I.

Sudan, Guinea-Bissau, Namibia, Gambia, Malawi na Jamhuri ya Afrika ya Kati pia ziliandikisha matokeo mazuri katika mechi hizo za Jumatano.

Katika mechi ya Senegal, wachezaji Sidy Sarr na Habibou Diallo, ambao wanasakata soka ya malipo nchini Ufaransa, walifunga mabao hayo muhimu dakika ya 26 na 28, mtawalia.

Senegal ilimaliza makala yaliyopita ya Afcon katika nafasi ya pili mwezi Julai, hii ikiwa ni mara yake ya pili kuambulia medali ya fedha katika mashindano haya. Haijawahi kushinda taji hili.

Mane na beki wa Napoli, Kalidou Koulibaly ni wachezaji nyota wa Senegal, inayotarajia kushinda kundi lake. Guinea-Bissau ilipepeta eSwatini yaani Lesotho 3-0 kupitia mabao ya Jorginho, Piqueti na Joao Mario jijini Bissau katika mechi nyingine ya kundi hili.

Nigeria, ambayo ilizoa nishani ya shaba kwenye Afcon nchini Misri mwezi Julai, ilitoka nyuma bao moja na kulipua majirani Benin 2-1 mjini Uyo.

Katika mechi hiyo ya Kundi L, veterani Stephane Sessegnon alipatia Benin bao la mapema katika dakika ya tatu.

Hata hivyo, Victor Osimhen alisawazisha 1-1 sekunde chache kabla ya kipindi cha kwanza kutamatika kupitia penalti kabla ya Samuel Kalu kuongeza bao la ushindi dakika ya 62.

Benin ilibandua miamba Morocco katika raundi ya 16-bora ya Afcon mwezi Julai na kutoa Senegal kijasho chembamba katika robo-fainali kabla ya kusalimu amri.

Katika mchuano mwingine wa kundi hili, Jane Thabantso alipokonya kinywani Sierra Leone kinywani aliposawazisha 1-1 dakika ya mwisho jijini Freetown. Kwame Quee alikuwa amepatia Leone Stars uongozi dakika ya 72. Wenyeji wa Afcon 2021, Cameroon, wanashiriki mechi hizi za kufuzu, kujipima nguvu. Walianza kampeni yao vibaya walipokabwa 0-0 na Cape Verde katika mechi ya Kundi F mjini Yaounde.

Indomitable Lions iliwasili nchini Misri mwezi Juni kama mabingwa watetezi, lakini ilipata ushindi mmoja pekee katika mechi nne na kubanduliwa nje ya kipute hicho na Nigeria katika raundi ya 16-bora. Matokeo hayo duni yalimfanya kocha Mholanzi Clarence Seedorf apigwe kalamu, huku Mreno Toni Conceicao akijaza nafasi yake na kusaidiwa na Francois Omam-Biyik.

Mvamizi matata wa Porto, Vincent Aboubakar alirejeshwa kikosini kuimarisha safu ya ushambuliaji, lakini Cape Verde ililinda ngome yake vyema na kutia kapuni alama moja muhimu.

Cape Verde itapigania tiketi moja kutoka kundi hili pamoja na Msumbiji na Rwanda zilizoratibiwa kumenyana Alhamisi usiku jijini Maputo.

Matokeo ya kushangaza

Matokeo ya kushangaza yalishuhudiwa jijini Luanda pale Gambia ilitoka chini bao moja na kuzima Angola 3-1 katika mechi ya Kundi D.

Baada ya Wilson Eduardo kuweka Angola kifua mbele dakika ya tatu, Assan Ceesay, ambaye anasakata soka yake nchini Uswizi, alifungia Gambia dakika ya 16 na 17 kabla ya Sulayman Marreh anayecheza nchini Ubelgiji kugonga msumari wa mwisho dakika ya 89. Kilikuwa kisasi kitamu kwa Gambia ambayo ililimwa nyumbani na ugenini na Angola miezi miwili iliyopita katika mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2022.

Sudan iliandikisha ushindi mkubwa Alhamisi ilipokung’uta Sao Tome e Principe 4-0 jijini Khartoum katika mechi ya Kundi C. Sao Tome e Principe ilikamilisha mechi watu 10 baada ya kipa wake nambari moja Aldair D’Almeida kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 22.

Namibia ilichabanga Chad 2-1 jijini Windhoek katika Kundi A, nayo Malawi ikalemea Sudan Kusini 1-0 jijini Blantyre katika Kundi B lililoshuhudia Uganda ikilazimisha sare ya 0-0 dhidi ya Burkina Faso jijini Ouagadougou. Jamhuri ya Afrika ya Kati ilizaba Burundi 2-0 jijini Bangui katika mechi ya Kundi E.

Mabingwa watetezi Algeria walialika Zambia mjini Blida katika mechi ya Kundi H ambapo walishinda 5-0. Zimbabwe na Botswana, ambazo pia ziko katika kundi hili, zinakabiliana leo Ijumaa jijini Harare.

Togo ilialika Comoros jijini Lome ambapo wageni walishinda 1-0 nayo Kenya ikatoka sare ya 1-1 na wenyeji Misri mjini Alexandria katika mechi za Kundi G.