Majagina wapiga tizi kali tayari kuvaana na Uganda

Majagina wapiga tizi kali tayari kuvaana na Uganda

NA JOHN ASHIHUNDU

WALIOKUWA wanasoka wa Harambee Stars wamezidisha mazoezi yao ugani City Stadium, Nairobi kujiandaa kwa ziara ya kwenda Uganda kwa mechi mbili za kirafiki.

Wakongwe hao chini ya kocha Robert Matano wamekuwa wakijiandaa kwa wiki moja na mazoezi hayo yanaendelea hadi juma lijalo kabla ya timu hiyo kuondoka Januari 24.

Matano aliye pia kocha mkuu wa timu ya Tusker FC alisema kikosi cha wachezaji 20 na maafisa watano watakuwa kwenye ziara hiyo.Jumatano, kikosi hicho kilipokea Sh200,000 kutoka kwa Twaha Mbarak anayewania kiti cha urais wa Shirikisho la Soka nchini (FKF).

“Mazoezi yetu yanajumulisha wachezaji wa umri tofauti, lakini watakaokubaliwa kucheza mechi ni walio na umri wa miaka 40 na zaidi. Tunatarajia wachezaji kadhaa waliokuwa wakijiandalia nje ya Nairobi kujiunga na timu mwishoni mwa wiki kwa maandalizi ya pamoja,” alisema mlinzi huyo wa zamani wa AFC Leopards.

Alisema kabla ya kuondoka kikosi hicho kitapimana nguvu na Wazito Wazee FC na baadaye Unattached Select FC.

Jumatano, kikosi hicho kilipokea Sh200,000 kutoka kwa Twaha Mbarak anayewania kiti cha Rais wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF).

Huku akiwaomba wamuunge mkono, Twaha alisema pesa hizo zitagharamia basi litakalowapeleka Uganda kwa mechi hizo.

“Mara tu nitakapotwaa mamlaka, nitahakikisha baadhi yenu mnahusika kikamilifi katika uimarishaji wa kandanda kuanza mashinani. Ningependa kuwaona wachezaji waliostaafu wakiwa mamlakani.”

Twaha alisema Kenya inazidi kubakia nyuma kutokana na ukosefu wa vituo vya kunoa vipaji, huku akiahidi kufufua vituo hivyo kote nchini.

“Tumepoteza mengi chini ya uongozi wa Nick Mwendwa kwa sababu watu wasiofaa walikuwa mamlakani, na sasa ni wakati wa wajumbe kuhakikisha wamechagua watu wanaofaa kuongoza mchezo huu. Tunahitaji umoja ili tufaulu katika jukumu hili,” aliongeza.

Twaha alitangaza kuwania kiti cha urais mwezi Novemba 2021, huku akimpteua aliyekuwa mwenyekiti wa jimbo la Magharibi Andrew Amukowa kama mgombea mwenza.

Alisema FKF inahitaji watu wapya watakaoleta pamoja washikaji dau wote kusaidia katika kuimarisha kandanda kote nchini.

“Nitahudumia Kaunti zote 47 kuimarisha kandanda kote nchini,” aliongeza Twaha ambaye amejumuisha wachezaji wengi wa zamani katika kampeni zao za kuwania kiti hicho.

Mbali na Matano, maafisa wengine wa kikosi cha Kenya ni Josephat Murila (kama meneja wa timu) na George Sunguti (kama naibu kocha).

Wengine walio kwenye kikosi hicho ni Musa Otieno, Dennis Oliech, Gabriel Olang’, Julius Owino, Vincent Otieno, Edward Karanja, Shadrack Ateka, Mohamed Fwaya, Zadock Shaban, James Nandwa, James Situma, Mike Otieno, Maurice Sunguti, Dancan Ochieng, George Maina, Mulinge Munandi miongoni mwa wengine.

  • Tags

You can share this post!

Kivumbi chanukia Boston Marathon ikivutia Kamworor, Bekele

TAHARIRI: Serikali ifanye juhudi kuzima mauaji ya watu

T L