Michezo

Majagina watuma rambirambi kumuomboleza kocha wa zamani wa timu ya Uingereza, Eriksson


NAHODHA wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza, David Beckham ni miongoni mwa wanasoka wastaafu waliotuma rambirambi zao kufuatia kifo cha kocha wa zamani wa timu hiyo, Sven-Goran Eriksson.

Kocha huyo aliyeaga dunia usiku wa kuamkia leo Jumanne, Agosti 27, 2024,  akiwa na umri wa miaka 76,  alimteua Beckham kuwa nahodha mara tu alipopewa jukumu la kunoa timu hiyo mnamo 2001.

Raia huyo wa Sweden alikuwa kocha katika mechi 59 za Beckham.

“Ulikuwa mtu mwenye shauku, mwenye kujali, mtulivu na muungwana wa kweli. Nitakukumbuka milele kwa kunipa jukumu la kuwa nahodha wa timu ya taifa,” alisema Beckham ambaye zamani alikuwa kiungo wa Manchester United na Real Madrid.

Mmiliki wa klabu ya Inter Miami nchini Amerika,  alituma ujumbe wake kupitia kwa mtandao wa kijamii ulioandamana na picha ya kuonyesha alipomtembelea mapema mwaka huu.

Eriksson alifariki kutokana na maradhi ya saratani ambayo yamesumbua kwa muda mrefu. Tulicheka, tukalia tukijua alikuwa anatuaga,” alisema Beckham.

Eriksson aliongoza timu ya Uingereza kufika robo-fainali ya mashindano matatu makubwa kati ya 2001 na 2006.

Kadhalika. alikuwa kocha wa klabu za Manchester City, Leicester City, AS Roma, Lazio, Fiorentina, Benfica, Sampdoria akishinda mataji 18 kwa jumla. Vile vile,  aliwahi kunoa timu za mataifa ya Mexico, Ivory Coast na Ufilipino.

Aliyekuwa mshambuliaji matata wa timu ya taifa ya Uingereza, Wayne Rooney,  alisema Eriksson alikuwa “mtu maalum”.

“Ulitusaidia na kutushuari. Asante kwa kumbukumbu. Pole zangu kwa marafiki na jamii,” aliongeza Rooney.

Nahodha wa sasa wa timu ya taifa ya Uingereza, Harry Kane alisema: “Sikupata fursa ya kucheza chini yake, lakini namuelewa kama mtu aliyependwa na kuheshimiwa na waliochezea timu yetu ya taifa akiwa kocha.

Mshambuliaji, Peter Crouch alisema: “Alikuwa mtu wa heshima zake. Alinipa nafasi kwa mara ya kwanza kuchezea timu ya taifa. Daima nitamkumbuka. Wengi watamkosa”.

Nahodha wa zamani wa timu hiyo, John Terry alimkumbuka marehemu kama kocha bora aliyejitolea katika kazi yake, huku kiungo wa zamani Frank Lampard,  akisema alikuwa kocha aliyeamini wachezaji wake.

Wengine waliotuma rambirambi zao ni pamoja na Micah Richards, Joe Hart, Kasper Schmeichel na Simone Inzaghi.

Kabla ya kustaafu kama mchezaji akiwa na umri wa miaka 27, Eriksson alianza kazi ya ukocha katika klabu ya Degerfors mnamo 1977 kabla ya kujiunga na klabu ya Gothenburg nchini Sweden na kuisaidia kutwaa ubingwa wa Uswidi, vikombe viwili vya Uswidi na Kombe la UEFA mnamo 1982.